Kampuni Ya Airtel Tanzania Imekubali Kutoa Baadhi Ya Hosa Zale Kwa Serikali Ya Tanzania.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 11 Januari, 2019 amekutana na Mwenyekiti wa kampuni ya Bharti Airtel Bw. Sunil Mittal, Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo wamezungumzia maendeleo ya mazungumzo ya umiliki wa hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.


Baada ya mazungumzo hayo Bw. Sunil Mittal amesema kampuni yake imekubali kuongeza hisa zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania katika kampuni ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49 na hivyo kupunguza hisa zilizokuwa zikimilikiwa na Bharti Airtel kutoka asilimia 60 hadi asilimia 51.
Bw. Sunil Mittal ameongeza kuwa mazungumzo kati ya kampuni yake na Serikali ya Tanzania yanakwenda vizuri na kwamba kampuni ya Bharti Airtel imeridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa katika masuala yaliyokuwa yakijadiliwa yenye lengo la kuiimarisha kampuni ya Airtel, kuleta manufaa kwa pande zote mbili na kuboresha huduma za mawasiliano za kampuni hiyo.


Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa katika mazungumzo hayo ambapo pamoja na kuongeza hisa za Serikali katika umiliki wa Airtel Tanzania, kampuni hiyo imekubali kutoa gawio kwa Serikali ya Tanzania mara baada ya mazungumzo hayo kukamilika hivi karibuni. “Masuala mengine ya kumalizia mazungumzo haya yataendelea leo ili kumalizia, lakini jambo zuri ni kuwa sasa wamekubali kutoa gawio kwa Serikali ambapo kwa muda wa miaka minane hadi kumi tulikuwa hatujapata gawio, kiasi cha asilimia za gawio nacho watajadili leo, kwa hiyo mimi naona huu ni mwanga mzuri wa kwenda mbele kati ya kampuni ya Bharti Airtel na Serikali ya Tanzania pamoja na kampuni zingine” amesema Mhe. Rais Magufuli.






No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.