Okwi: Pointi Tatu Ni Muhimu Kwetu


Mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Emmanuel Okwi, amesema wamejipanga kuikabili Yanga kwa kasi na nidhamu ya hali ya juu ili kutimiza malengo yao ya kushinda mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ushindi utaiweka Simba katika nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa wa msimu huu.

Okwi, raia wa Uganda alisema mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kama zilivyo mechi nyingine za ligi hiyo, lakini timu itakayojipanga kutumia vyema nafasi watakazotengeneza ndiyo itafanikiwa kuondoka na pointi tatu.

Okwi, kinara wa kupachika mabao msimu huu akiwa ameshatupia 19, alisema atafurahi zaidi kuona wanapata pointi tatu katika mechi hiyo ya marudiano bila kujali ni mchezaji gani atafanikiwa kufunga bao ama mabao.

"Ni mechi ngumu kama nyingine, tofauti ni pale huo ni mchezo wa 'derby' (watani), lakini nguvu na mbinu ni zile zile tunazozitumia kila siku, tunajituma ili kuwapa furaha mashabiki wetu wa Simba," alisema mshambuliaji huyo.

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 59 baada ya kucheza mechi 25, huku wakifuatiwa na mabingwa hao watetezi wenye pointi 48, lakini wamecheza michezo 23.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.