Mhilu Huyu Alikuwa Wapi?


Kiwango kinachoonyeshwa na winga chipukizi Yusuph Mhilu kimeendelea kuinufaisha Yanga kwa kuisaidia kupata matokeo katika michezo muhimu.

Mhilu alirejea rasmi kwenye kikosi cha kwanza baada ya kufanya vizuri katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom dhidi ya Kagera Sugar mchezo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku yeye akifunga moja ya mabao hayo uwanja wa Taifa.

Baada ya mchezo ule, Mhilu amejihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza na hakika hajamwangusha kocha George Lwandamina ambaye sasa anamuamini kwa asilimia 100.

Wengi wamekuwa wakijiuliza Mhilu alikuwa wapi siku zote? Kwani kama angeanza msimu na kasi hii aliyonayo sasa, bila shaka angekuwa ameisaidia zaidi Yanga.

Mwanzoni mwa msimu Yanga iliathiriwa sana na pengo la Saimoni Msuva lakini kama Mhilu angekuwa katika kiwango alicho sasa hali ingekuwa tofauti.

Faida zaidi ya Mhilu ni uwezo wake wa kucheza winga zote na hata nafasi ya ushambuliaji wa kati.

Anapocheza pembeni mipira yake mingi ya krosi imekuwa na madhara makubwa na kuizalishia mabao Yanga.

Katika mchezo dhidi ya Wolaitta Dicha krosi yake murua ilizaa bao la pili la Yanga lililofungwa na Emanuel Martini.

Mhilu pia ndiye aliyemtengea pasi murua Haji Mwinyi ambaye alimimina majaro iliyozaa bao la kwanza lililofungwa na Raphael Daudi

Sasa anaonekana kujiamini na kufanya maamuzi sahihi mara nyingi anapokuwa na mpira. Mambo haya hakuwa nayo mwanzoni mwa msimu. 

Katika moja ya mahojiano yake akizungumzia mafanikio yake tangu arejee kwenye kikosi cha kwanza cha yanga, Mhilu alisema kikao walichofanya na benchi la Ufundi baada ya wachezaji wengi kuwa majeruhi ndicho kilichopelekea kumfanya ajiamini zaidi.

"Binafsi nina kila sababu ya kuipigania timu yangu ya Yanga baada ya wao kuniamini," alisema Mhilu 

"Baada ya kuona wachezaji wale wakubwa wamekuwa majeruhi wa muda mrefu na wao ndiyo walikuwa wanategemewa, sisi vijana tulikalishwa chini na kuambiwa ndiyo wa kwenda kuikoa Yanga na hivyo tukapambane".

Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.