Lipuli kumaliza kwa kishindo michezo nane iliyobaki VPL
Klabu ya soka ya Lipuli ya mjini Iringa, imesema imedhamiria kumaliza kwa kishindo michezo nane ya ligi kuu soka Tanzania Bara ili kuweka heshima wanapoingia katika msimu ujao wa ligi.
Akizungumza na mtandao huu Msemaji wa klabu hiyo, Clement Sanga amesema kwa kuwa wamedhamiria hayo kwa sasa kikosi chao kikiwa chini ya kocha Amri Said na Seleman Matola kinafanya mazoezi mara mbili kwa siku kwa takribani majuma mawili kabla ya safari ya kwenda Mwanza waliyoifanya Jumanne asubuhi.
"Toka tuliporudi kwenye likizo tumekuwa tukifanya mazoezi mara mbili kwa siku, lengo letu ni kuwaweka wachezaji wetu katika utimamu wa akili na mwili, ili kumaliza michezo yetu iliyobaki, na mchezo uliopo usoni ni dhidi ya Mbao April 6, 2018 kule Mwanza," Sanga amesema.
Hakuna majeruhi
Sanga ameendelea kusema kuwa hali ya kikosi ipo vizuri kwani hakuna hata mchezaji ambaye ana majeraha yanayoweza kumuweka nje ya uwanja kwa siku za hivi karibuni.
"Nimezungumza na daktari wa timu hakuna majeruhi hata mmoja, kikosi chote kipo sawa sawa, na tumeondoka na wachezaji 24 kuelekea huko Mwanza asubuhi ya jumanne na hii ni kwa ajili ya michezo miwili ya kanda ya ziwa dhidi ya Mbao na Mwadui FC," Sanga amesema.
Kwa sasa Lipuli wapo nafasi ya saba wakiwa na alama 27 katika msimamo wa ligi kuu soka Tanzania Bara.
Aidha wamebakiwa na michezo nane kumaliza ligi ambayo ni dhidi ya Mbao, Mwadui, Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar ambayo watacheza ugenini na ile dhidi ya Simba SC, Mbeya City, Kagera Sugar na Singida United ambayo watacheza katika uwanja wao wa nyumbani wa Samora.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.