TFF YAFUTA TUZO YA MCHEZAJI BORA WA KIGENI LIGI KUU.
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefuta tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo mwaka jana ilichukuliwa na kiungo Mzimbabwe wa Yanga, Thabani Scara Kamusiko.
Taarifa ya TFF iliyotolewa na Msemaji wa shirikisho hilo, Clifford Ndimbo imesema kwamba shere za Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu zitafanyika Juni 23 mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
“Kufanyika kwa tuzo hizo ni utaratibu ambao Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limejiwekea kila mwaka baada ya kumalizika ligi kutoa tuzo kwa waliofanya vizuri kwa kushirikiana na Wadhamini wakuu wa VPL Kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom Plc na msimu huu tutakuwa na washirika wengine Azam Tv, Benki ya KCB na Premier Bet,”amesema Ndimbo.
Licha ya Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka wa ligi, pia kunatolewa tuzo mbalimbali, ambapo kwa mwaka huu tuzo moja imeondolewa na nyingine imeongezwa ikiwa ni katika kuboresha.
Tuzo iliyoondolewa ni ya Mchezaji Bora wa Kigeni na imefanyika hivyo ili kuwapa fursa wachezaji wote kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL badala yakuwatenganisha.
Pia msimu huu imongezwa Tuzo ya Mwamuzi Bora Msaidizi ambayo haikuwepo msimu uliopita, hiyo ni kutokana kuthamini nafasi ya waamuzi wasaidizi.
Kwa mazingira hayo tuzo zitakazotolewa Juni 23, ambapo wadhamini wakuu ni Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ni hizi Bingwa, Mshindi wa Pili, Mshindi wa Tatu, Mshindi wa Nne, Mfungaji Bora, Timu yenye nidhamu, Mchezaji Bora chini ya umri wa miaka 20, aambayo imepewa jina la Tuzo ya Ismail Khalfan, Mchezaji Bora Chipukizi, Mwamuzi Bora Msaidizi, Mwamuzi Bora, Kipa Bora, Kocha Bora, Bao Bora, Kikosi Bora cha Wachezaji 11 wa Ligi Kuu na Mchezaji wa Heshima.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.