KOCHA LIPULI AWALALAMIKIA WALIOMZUSHIA KUUZA MECHI
Kocha msaidizi wa timu ya Lipuli FC, Suleiman Matola amelalamika kuwa kabla ya mchezo wao dhidi ya Simba hapo jana alizushiwa kuchukua pesa kwa Wekundu hao ili kuuza mechi iliyomalizika kwa sare ya bao moja.
Kabla ya mechi iliyochezwa uwanja wa Samora, Iringa kulikuwa na picha zilizokuwa zikizagaa mitandaoni Matola akiwa na baadhi ya wachezaji na viongozi wa Simba zilizopigwa wakati Wekundu hao wakijiandaa na mechi ya Njombe Mji.
Matola ambaye aliwahi kuwa nahodha wa timu ya Simba alisema alisikitishwa na tuhuma hizo lakini kiwango walicho onyesha kimewazima watu midomo.
"Kulikuwa na taarifa kuwa nimepokea pesa za Simba niwape wachezaji wangu ili tufungwe kitu ambacho kimeniuma sana.
"Lakini kilichotokea kila mtu ameona tuliwadhibiti kila idara na tulikuwa na uwezo wa kufunga sema bahati ilikuwa upande wa Simba," alisema Matola.
Hata katika mchezo wa kwanza uliofanyika katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kocha huyo alizushiwa kuchukua pesa ili kuuza mechi lakini mechi iliisha kwa sare ya bao moja.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.