Yanga Waitandika Kagera Sugar Waipumulia Simba Kileleni..


Ligi kuu soka Tanzania raundi ya 22 mzunguko wa kwanza imeanza kwa kasi kwa Mabingwa watetezi Dar Young Africans kuibuka na ushindi muhimu wa mabao 3-0 dhidi ya wanankurukumbi Kagera Sugar.

Mchezo huo ambao umefanyika katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam umemaanisha kwamba Yanga wamezidi kuisogelea Simba kileleni, kwani kwa sasa tofauti ya alama baina yao zimebaki tatu kutoka saba za hapo awali.

Mchezo huo ambao ulikuwa mkali kwa kila upande kulishambulia lango la mwenzake, na kushuhudia kosa kosa za hapa na pale huku kipa wa Kagera Sugar Ramadhan Chalamanda akiokoa michomo hatari ya wachezaji Emmanuel Martin na Ibrahim Ajib.

Mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko hakukuwa na timu yoyote ambayo ilifanikiwa kupata bao, huku Yanga wakionekana kuwa na asilimia kubwa za umilikaji wa mpira zaidi ya wageni Kagera Sugar.

Mabao ya Yanga
Yanga walipata bao la kwanza katika dakika ya 51 baada ya mwamuzi Shomari Lawi kuamuru penati baada ya mlinzi wa Kagera Sugar Mohamed Fakhi kunawa mpira ndani ya 18 akiwa katika juhudi za kuokoa shuti la Emmanuel Martin.

Penati hiyo ilikwenda kuchongwa na Ibrahim Ajib Migomba ambaye alipiga upande wa kulia wa mlinda mlango Ramadhan Chalamanda na kuandika bao la kuongoza kwa mabingwa hao watetezi.

Bao la pili katika mchezo huo lilifungwa katika dakika ya 77 baada ya walinzi kujisahau na kuruhusu krosi ya Ibrahim Ajib kumfikia Obrey Chirwa ambaye bila kutuliza alipiga V-Pass iliyomkuta Emmanuel Martin na kuukwamisha mpira nyavuni.

Yanga walipata bao la tatu baada ya kazi nzuri ya Yusuf Mhilu ambaye alipanda na mpira kwa kasi na kutoa pasi ambayo katika juhudi za kuuokoa mlinzi wa Kagera Sugar Juma Shemvuni alijikuta akimpoteza maboya kipa wake na mpira huo ukajaa kimiani.

Matokeo hayo yanawafanya Yanga kufikisha alama 43 na kukalia nafasi ya pili nyuma ya alama tatu dhidi ya Simba ambao wao wana alama 46 wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi, wakati ambapo timu zote zimekwishakucheza mechi 20.

Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.