Wachezaji Simba Wamwagiwa Mifedha Kuimaliza Al Masry
Mabosi wa Simba wakiongozwa na Bilionea, Mohammed Dewji, wameanza mikakati ya kuwamaliza Al Masry kwa kuongeza motisha ya posho kwa wachezaji wao katika mechi za kimataifa ambazo watashinda.
Kwenye ligi kuu, utaratibu uliopo wakishinda kila aliyecheza anapewa Sh300,000 awahi nyumbani huku waliokaa benchi wakivuta Sh200,000 na waliokaa jukwaani wanaondoka na Sh150,000.
Sasa habari njema kwa nyota hao ni kwamba kwenye mechi za kimataifa, timu ikishinda waliocheza watavuta Sh400,000 na kitita kinaweza kuzidi kwa mtu hadi kufikia Sh500,000 kutokana na kiwango atakachoonesha.
Wachezaji watakaokaa benchi kimataifa kila mmoja atapata Sh300,000 lakini itakuwa maumivu kwa watakaokaa jukwaani kwenye mechi hizo za kimataifa kwani hawataambulia kitu.
“Mashindano haya ni magumu na tunatamani kufanya vizuri kama tunavyofanya katika ligi, ndio maana tumeongeza posho ili kila mchezaji atamani kucheza kwa nguvu na kuisadia timu, pia kutimiza malengo yake,” kilisema chanzo chetu.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.