Unaambiwa Posho za wachezaji wa Rollers zinalipa mishahara ya wachezaji wa Yanga kwa miezi miwili na zaidi

Mwenye pesa usishindane naye. Yanga mbali na kupigiwa soka safi na Township Rollers juzi Jumanne, nje ya uwanja wageni hao kutoka Botswana walichoma mkwanja wa maana.


Yanga ilichapwa mabao 2-1 na Wabotswana hao katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kuzima ndoto za kusonga mbele licha ya kwamba watarudiana ugenini siku 10 zijazo.


Uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti umebaini kwamba uongozi wa Township Rollers chini ya Bilionea Jagdish Shah ambaye ni Rais wa timu hiyo, umelazimika kutumia kiasi cha Dola 115000 (kama Sh.260milioni) kuwapatia wachezaji 23 waliosafiri na timu hiyo kuja jijini kucheza mechi hiyo, hizo zikiwa ni posho tu.


Habari hizo ambazo zilithibitishwa na Bickie Mbenge ambaye ni mmoja wa maofisa waliombatana na timu hiyo, zimebainisha kwamba kutokana na umuhimu na ugumu wa mechi ya ugenini dhidi ya Yanga, uongozi wa Township Rollers uliwapa ahadi ya kutoa Dola 5,000 (Sh. 11 Milioni) kwa kila mchezaji iwapo timu hiyo itaibuka na ushindi.


Idadi ya wachezaji ambao walikuwemo kwenye msafara wa timu hiyo ilikuwa ni 23, namba ambayo ukizidisha kwa Dola 5000 iliyotolewa kwa kila mchezaji, unapata kiasi cha jumla kilichotumika kwa wachezaji pekee kufikia Dola 115,000 kama kifuta jasho kwa kufanya kazi kubwa ya kuibuka na ushindi ugenini.


Kiasi hicho cha fedha kinaweza kuzidi iwapo bonasi hiyo itawahusisha pia maofisa wa benchi la ufundi ambao walikuwemo kwenye msafara wa timu hiyo ambao ulifikia kwenye hoteli ya kifahari ya Southern Sun iliyopo Posta Jijini.


Sasa unaambiwa mishahara ya wachezaji wote wa Yanga na benchi la ufundi hauzidi Sh 120 milioni hivyo fedha hizo zingeweza kulipa mishahara ya miezi miwili pale Jangwani na chenchi ikabaki.


"Huu ni utaratibu ambao tumeuweka kwa lengo la kuwapa hamasa zaidi wachezaji wetu ili tuweze kufanikiwa kufika mbali na kufanya vizuri kwenye mashindano haya ya ngazi za klabu Barani Afrika.


Kama unavyoona timu yetu imekuwa ikifanya mambo kisasa zaidi na pasipo kutumia fedha ni vigumu kuweza kushindana na timu za Afrika Kaskazini ambazo zimefanya uwekezaji wa hali ya juu," alisema Mbenge.
Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.