Singida Utd waitangazia kiama Yanga
Timu ya soka ya Singida United imeendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa robo fainali ya Kombe la Azam Sports Federation Cup dhidi ya Mabingwa wa zamani Dar Young Africans utakaofanyika April Mosi kwenye uwanja wa Namfua mjini Singida.
Singida united ambao wamelazimika kutoka nje ya mji wa Singida na kuweka kambi katika Mji mdogo wa Kiomboyi, wanafanya mazoezi mara mbili kujiandaa na mchezo huo muhimu.
Meneja wa Singida United Ibrahim Mohamed amesema kikosi kipo vizuri na kutokana na kuiheshimu Yanga wameona wasogee nje ya mji wa Singida na wataendelea na mazoezi huko hadi Jumamosi watakaporejea mjini Singida.
"Maandalizi yapo vizuri na kweli tumetoka nje kidogo ya mji wa Singida, tumesogea kidogo maeneo ya Kiomboyi, kila kitu kipo vizuri ni mchezaji mmoja tu ambaye ana majeraha Salumu Kipaga na anajiunga na wenzake Jumatano, hivyo wachezaji wote wapo vizuri, tutaendelea na mazoezi mpaka Jumamosi tutarejea Singida mjini," Mohamed amesema.
Watatusamehe
"Daima unapokutana na Yanga unakutana na timu kubwa, tumecheza nao mara nne, wametufunga mara moja katika mchezo wa kirafiki, michezo mingine tumetoka nao sare, tunawaheshimu sana lakini mara hii watatusamehe, tunahitaji matokeo ili tusonge mbele," ameongeza.
Aidha Ibrahim amesema kocha Hans Van der Pluijim amesema anaumia kuona anapoteza mchezo katika timu ambayo awali aliwahi kuifundisha hivyo amejipanga kimbinu na kiufundi kuhakikisha anaifunga Yanga na kusonga mbele.
Mchezo huo utatoa mshindi ambaye atakutana na mshindi kati ya Tanzania Prisons na JKT Tanzania
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.