Ipi nafasi sahihi ya Mbwana Samatta Stars
Na Baraka Mbolembole
KUNA uzuri gani kwa mchezaji ambaye asili yake ni ushambuliaji kucheza mbali na goli la wapinzani kwa mita 30 hadi 50? Baada ya kichapo cha 4-1 kutoka kwa Algeria siku ya Alhamisi iliyopita kumekuwa na mijadala tofauti kuhusu uwezo wa kiufundishaji wa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Salum Mayanga na mwenendo mzima wa kikosi chake.
Mara baada ya kocha msaidizi, Hemed Morocco kutangaza orodha ya wachezaji wa Stars watakaozivaa Algeria (umeshachezwa) na DR Congo (itachezwa Jumanne hii) katika michezo ya Kimataifa-kalenda ya Fifa, nilitazama na kuhoji kuhusu uwepo wa Thomas Ulimwengu, Farid Musa na kukosekana kwa majina ya Jonas Mkude na Pius Buswita.
Wapo pia walioulizia kutokuitwa kikosini kwa Habib Haji Kiyombo, Rashid Mandawa, Nurdin Chona na baadhi ya wachezaji wanaoonekana kufanya vizuri hivi sasa.
Ukosoaji huu ulifika mbali zaidi kiasi cha kusemwa kocha Mayanga amekuwa akichaguliwa wachezaji na ‘watu wasiojulikana’ jambo ambalo alikuja kulikanusha haraka baada ya kipigo kutoka kwa ‘Mbweha wa Jangwani‘ wiki iliyopita. Kukoselewa sana kwa teuzi za vikosi vya timu ya Taifa hakukuanza leo, wala si Tanzania pekee.
Mgongano wa namna hii itaendelea kutokea hadi kwa ‘wafalme wa kandanda‘ duniani-Brazil. Matokeo siku zote hutoa ukweli, ndio maana licha ya kuitwa kikosini kwa Mandawa baada ya shinikizo, Mayanga wala hakumpa nafasi ya kutosha mshambulizi huyo katika mfumo wa 4-4-2 dhidi ya Algeria huku mbinu zake zikiongozwa na upangaji mbaya wa kikosi.
Kumuacha nje erasto nyoni
Mayanga aliwaanzisha mabeki wanne. Shomari Kapombe katika beki ya kulia, Gadiel Michael beki-tatu, Abdi Banda na Kelvin Yondani katika beki ya kati. Wote hawa yalikuwa ni machaguo mazuri, lakini kama Mayanga angemuanzisha Erasto Nyoni katika nafasi aliyoanza Himid Mao Stars isingefungwa goli la pili alilojifunga Kapombe dakika chache kabla ya Half-time. Kama lengo ilikuwa ni kujifunza, basi Mayanga hakupata funzo lolote Algeria na badala yake amejionyesha alivyo ‘mtu wa kubahatisha’ kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Charles Boniface Mkwasa ambaye kikosi chake kilichapwa 7-0 na Mbweha hao katika mchezo wa kufuzu WC2018 miezi karibia 16 iliyopita.
Nadhani Mayanga alipaswa kuicheza Stars katika mfumo wa 5-3-2. Mara nyingi Stars na hata vilabu vyetu vimekuwa vikipoteza michezo ya ugenini dhidi ya timu za Kiarabu na zile zinazotoka nchi zenye mafanikio zaidi yetu katika soka la Afrika, hivyo tulipaswa kupima uwezo wetu hasa katika kujilinda na vile tuna ratiba ya kucheza nyumbani na timu nyingine kubwa Afrika, Jumanne hii vs DR Congo tunapaswa kupima uwezo wetu wa kujilinda, kupanga mashambulizi na kufunga magoli.
Kuwapanga, Kapombe, Gadiel, Banda, Kelvin na Erasto katika safu ya walinzi watano dhidi ya Algeria, Mudathir Yahya, Said Ndemla na Saimon Msuva kama viungo watatu wenye jukumu la kuunganisha timu kutokea nyuma hadi safu ya mbele, na kupanga mashambulizi kuelekea kwa Mandawa na nahodha Mbwana Samatta ni jambo ambalo lingekuwa na maana sana-tungejua uwezo wa timu yetu katika kujilinda ugenini dhidi ya timu kubwa.
Lakini tumechapwa 4-1 na wakati tunasubiri uchambuzi wa kiufundi kutoka kwa Mayanga-kocha ameishia kusema: “Sijachaguliwa timu.”
Hakuna tulichojifunza, ila ninaendelea kuziona sababu zenye mashiko ambazo zinatuumiza kila wakati.
Kwa wachezaji aliokuwa nao Algeria, Mayanga ilikuwa lazima aegemee katika mbinu za kiulinzi zaidi na kutegemea maarifa binafsi ya kina Ndemla, Mudathir, Msuva na Samatta kuchezesha na kulinda mbinu zake.
4-4-2 iliyowaweka pamoja Himid na Mudathir katika kiungo cha kati, ingefaa zaidi vs DR Congo. Hapana shaka kuhusu uwezo wa Himid anapokuwa fiti kimwili na kiakili, lakini kwa dakika zote 45 za kwanza alikuwa hovyo katika upigaji pasi, kukaba na kupandisha timu.
Alimtesa sana Mudathir aliyelazimika kucheza karibia mita tano ya mahala alipokuwa Himid, zaidi alimpa mateso Gadiel kutokana na kupoteza sana mpira huku pasi zake nyingi zikikosa mwelekeo. Himid hakuwa fit na pengine alihitaji walau dakika 15 tu vs Algeria.
Kushindwa kumtumia Samatta
Katika umri wa miaka 25-27 mchezaji anakuwa anaingia katika sehemu ya pili ya maisha yake ya soka. Kuendelea kumchezesha Samatta mbali na goli ni sawa na kuanza kumfunza upya, na kwa umri wake wa miaka 25 haiwezi kutokea haraka akabeba jukumu la mchezesha timu.
Kwa mchezaji aliyetumia dakika chini ya 15 kufunga goli lake la kwanza katika mchezo wa kwanza wa kimataifa akiwa U19 miaka saba iliyopita ingependeza kukuta sasa ana walau magoli 25-30 katika wasifu wake timu ya Taifa.
Sishangazwi na ‘sura ya huzuni‘ ya Samatta anapomaliza mechi ya Stars bila kufunga goli, huku wachezaji wengine wakifunga na kujaribu kuisaidia timu. Kabla ya majeraha Samatta ndiye alikuwa mshambulizi namba moja wa klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji Inashangaza kiasi kuona mchezaji bora kama huyu kiufungaji akichezeshwa mbali la goli katika Taifa lenye uhaba mkubwa wa wafungaji.
Kuna wakati Mkwasa alikuwa akiwachezesha Elius Maguli na Samatta katika mfumo wa 4-4-2 na angalau hapa Samatta alionyesha kufurahi. ‘Mimi ni namba 10゛amewahi kuniambia Samatta katika moja ya mahojiano niliyowahi kufanya naye.
Huu ndio ukweli, na licha ya kupenda kucheza karibu na lango la wapinzani, Samatta hafurahii kuchezeshwa kama mshambulizi wa kwanza. Yeye anapenda kucheza kwa uhuru eneo lote la mbele, kumtengenezea nafasi mshambulizi wa kwanza, na kufunga magoli muhimu.
Samatta kuna wakati ameshaonyesha kiwango bora akichezeshwa namba 10-rejea, Ivory Coast 2-0 Stars, Stars 3-1 Morocco, Stars 2-2 Algeria na mara ya mwisho Stars 2-0 Botswana yapata mwaka mmoja uliopita.
Nadhani kocha Mayanga anapaswa kutazama upya mahala sahihi pa kumchezesha Samatta kwa faida ya timu na mchezo wake.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.