Yanga Wamalizana Na Refa Mapema Kuelekea Game Ya Kesho.


MABOSI wa Yanga wajanja sana kwani kwa kutambua wana mchezo mgumu kesho Jumatano, wamefanya mambo mawili ya maana ambayo kwa kiasi kikubwa yameiweka vizuri kisaikolojia timu yao tayari kuwamaliza St. Louis.

Kwanza, Kiongozi wa Msafara aliye Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika na Meneja wa timu hiyo, Hafidh Salehe, walimnasa mapema refa wa mechi hiyo, Andofetra Rakotojaona kutoka Madagascar kabla hata hajafika Shelisheli na kupiga naye stori mbili tatu ambazo zilimfanya atabasamu muda wote.

Awali Yanga walianza kuingia wasiwasi baada ya kufahamu Rakotojaona ndiye atachezesha mechi yao wakihisi ndiye aliwafanyia roho mbaya mwaka juzi kwenye mchezo wao dhidi ya SD Esperanca ya Angola katika Kombe la Shirikisho ambapo alitoa kadi nyekundu ya kushangaza kwa Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Lakini kinyume na mawazo ya Yanga, Rakotojaona hakuchezesha pambano hilo la Angola na badala yake alikuwa ni Hamada Nampiandraza.

Wasiwasi huo uliwafanya Nyika na Hafidh kumvaa Rakotojaona na wenzake wanne pindi walipokutana nao Uwanja wa Ndege jijini Nairobi, walipokuwa wakisubiri ndege ya kuunganisha kuja Shelisheli ambapo waliwasalimia na kuzungumza nao kwa kifupi huku marefa hao wakionyesha kuwachangamkia na kuwapa ushirikiano.

Mbali ya kuzungumza nao, pia Yanga ilisafiri pamoja na Rakotojaona aliyekuwa na wasaidizi wake, Lionel Hasinjarasoa Andrianantenaina sambamba na Pierre Jean Eric Andrivoavonjy waliopewa jukumu la kuchezesha mechi hiyo.

Lakini kingine ni akili ya kuzaliwa ambayo Nyika na Katibu wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Samuel Lukumay waliitumia kuipeleka timu nje kidogo ya mji ambako hakuna msongamano wala mwingiliano wa watu unaoweza kuwafanya wachezaji wasiwe kwenye utulivu.

Yanga imefikia Hoteli ya Reef Holiday iliyopo upande wa Mashariki mwa mji mkuu wa Shelisheli, Victoria, eneo ambalo ni mwendo wa dakika zisizozidi 15 tu kwa gari kutoka ulipo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mahe.

Ni eneo lililo jirani kabisa na ufukwe wa bahari ya Hindi ambalo limezungukwa na miti inayofanya kuwe na mandhari ya kuvutia pamoja na hali ya hewa tulivu kama ilivyo maeneo ya Masaki, Dar es Salaam.

Kutokana na hofu ya hujuma, viongozi hao kwa kuzingatia ushauri wa Daktari, Edward Bavu na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Issa Bukuku, waliamua kugomea chakula cha hotelini hapo na kwenda kukisaka mahali pengine huku wakifanya utaratibu wa kutafuta sehemu maalumu ya kupikia.

TIZI KALI

Yanga jana ilipiga tizi kwenye Uwanja wa Stade Linite, ikitumia masaa mawili kuanzia saa 9-11 kwa saa huku ambazo ni sawa na saa 10-12, huku Kocha George Lwandamina akiwapa mbinu nyota wake kutengeneza nafasi za mabao kupitia mashambulizi ya pembeni yakiaanzia.

Kocha Msaidizi, Shadrack Nsajigwa alisema lengo lao ni kuhakikisha kesho wanatoka na ushindi na kusonga mbele katika mechi za CAF.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.