Kairuki miaka mitatu, wizara tatu


RAIS John Magufuli jana alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na uteuzi wa viongozi mbalimbali wa wizara na taasisi za serikali huku Angellah Kairuki akiteuliwa kwa mara ya tatu kuwa waziri tangu mwaka 2015.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki picha mtandao
Katika uteuzi huo uliotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, balozi John Kijazi, Ikulu jijini Dar es Salaam, Kairuki amekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.

Kijazi katika taarifa hiyo ya uteuzi, alikaririwa akisema Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Waziri anayeshughulikia masuala ya uwekezaji kwa lengo la kuongeza msukumo na kuimarisha usimamizi wa masuala ya uwekezaji hasa baada ya kuamua Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuhamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kabla ya uteuzi huo, Kairuki alikuwa Waziri wa Madini, nafasi ambayo aliitumikia tangu mwaka jana baada ya Rais kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri ikiwa mara ya pili kuteuliwa kwake kuwa waziri. Mara ya kwanza aliteuliwa Desemba, 2015 kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kutokana na mabadiliko hayo ya Kairuki, Rais Magufuli amemteua Doto Biteko aliyekuwa Naibu Waziri katika wizara hiyo kuwa Waziri wa Madini.

“Awali, wizara hiyo ilikuwa na naibu mawaziri wawili, Biteko na Stanslaus Nyongo na sasa itabaki na Naibu Waziri mmoja, Nyongo, ambaye ataendelea na wadhifa wake,” alisema Balozi Kijazi.

Sambamba na mabadiliko hayo kwenye baraza la mawaziri, Rais aliteua makatibu wakuu kwa kumteua Mhandisi Joseph Nyamuhanga kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Kabla ya uteuzi huo, Nyamuhanga alikuwa Katibu Mkuu Ujenzi na anachukua nafasi ya Mhandisi Mussa Iyombe ambaye amestaafu utumishi wa umma.

Mwingine aliyeteuliwa ni Dk. Zainabu Chaula kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia afya). Kabla ya Uteuzi huo, Dk. Chaula alikuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (anayeshughulikia Afya).

Naye Elius Mwakalinga ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi. Kabla ya uteuzi huo, Mwakalinga alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Aidha, Dorothy Mwaluko kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji). Kabla ya Uteuzi huo Bi. Mwaluko alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Pia Dk. Dorothy Gwajima ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia Afya. Kabla ya uteuzi huo Dk. Gwajima alikuwa Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Francis Michael, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

ATEULIWA BALOZI

Katika mabadiliko yaliyofanywa na Rais jana, Dk. Mpoki Ulisubisya ameteuliwa kuwa Balozi na kituo chake cha kazi kitatangazwa baadaye. Kabla ya uteuzi wa jana, Dk. Ulisubisya alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (akishughulikia afya).

Pia Prof. Faustin Kamuzora kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Diwani Athumani ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Viongozi hao walioteuliwa wanatarajia kuapishwa leo saa 3:30 asubuhi, Ikulu jijini Dar es Salaam.

NAFASI YAFUTWA

Pamoja na kuteua viongozi katika nafasi hizo, Rais Magufuli amefuta nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi ya Kujenga Taifa, hivyo kubaki na Katibu mkuu pekee. Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa Immaculate Ngwalle ambaye amestaafu.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amefanya uamuzi wa kufungua ubalozi mpya wa Tanzania nchini Cuba na mwakilishi katika nchi hiyo atateuliwa baadaye.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.