Mkwara wa kocha Simba wawashitua Mabosi na kupelekea kufanya jambo hili.


MABOSI wa Simba wameshtushwa na mkwara uliopigwa na Kocha Mkuu, Patrick Aussems na sasa hata kabla ya Mbelgiji huyo hajatua nchini na kikosi chake kutoka kambini Uturuki, uongozi umepanga kufanya mambo mawili ya kumtuliza kocha huyo.
Wakuu wa Wekundu wa Msimbazi hao wameamua kutimiza sharti moja zito ambalo kocha huyo amewapa ili aiongoze timu hiyo kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa, pia wameamua kumpa zawadi nyingine itakayomrahisishia kazi Aussems.
Kocha huyo ameitaka Simba kuhakikisha inakuwa na uwanja mzuri wa kudumu wa mazoezi, jambo ambalo uongozi wa timu hiyo umeahidi kulifanyia kazi siku chache zijazo kwa kuanza ujenzi wa uwanja wake uliopo Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Lakini wakati wakijipanga kuanza mchakato wa ujenzi huo, klabu hiyo imeamua kumpunguzia majukumu Aussems kwa kupanga kumleta mtaalamu wa tathimini ya mechi atakayemsaidia Mbelgiji huyo kufanya maamuzi sahihi ya kiufundi pindi wanapocheza mechi za mashindano mbalimbali.
Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema suala la mchakato wa ujenzi wa uwanja halitochukua muda mrefu kutokana na shinikizo kutoka benchi lao la ufundi.
“Kocha wetu hakubali kupeleka wachezaji kwenye viwanja visivyo na ubora, lakini vile vizuri vyenye ubora tunavikodi kwa gharama kubwa na sisi tulichokipanga kwa sasa ni kupunguza gharama hizo,” alisema.
“Fedha za kujenga uwanja tunazo ila kuna baadhi ya mambo yalikuwa yanatukwamisha mfano suala la kesi iliyoko mahakamani.
“Ninachotaka kusema ni kwamba watu wawe na subira, mwezi huu wa Agosti hautomalizika. Tukimaliza Simba Day tunakwenda Bunju. Hilo ndilo tunalotaka kulifanya kwa sasa, Simba ni klabu kubwa hivyo ni lazima kuwa na uwanja wetu.”
Try Again alisema mbali ya mipango hiyo ya uwanja, wamejipanga kuongeza ufanisi kwenye benchi la ufundi kwa kumwongeza mtaalamu wa kusoma mchezo ili Simba iweze kufanya vizuri.
“Sisi tumejipanga kwa hali yoyote kwa sababu hatujui tutakutana na nani. Atakayekuja mbele yetu tutapambana naye. Klabu za Kaskazini na nyingine zinazoonekana tishio, tuko nazo katika daraja moja kama ni utofauti basi ni mdogo tu,” aliongeza.
“Mashindano ni mkakati. Unapokwenda kushindana sio unakwenda tu, bali unatakiwa kujipanga. Mechi za kimataifa zinachezwa kwa mikakati. Unacheza na nani, wapi na saa ngapi. Unayecheza naye anachezaje? Simba sasa tunaajiri mtu anayeitwa ‘Match Analyser’ (Mtathmini wa Mechi).
“Kazi yake ni kusoma mchezo. Muda wote anautazama na kumpa taarifa kocha kuwa hawa wapinzani wanafungika vipi, wanachezaje na wanabadilika vipi. Hapo kocha atajua ili kuweza kushinda ni lazima afanye maandalizi yapi, hiyo ni kutanua benchi la ufundi.”
Kwa sasa benchi la ufundi la Simba linaundwa na watu saba ambao ni Aussems, Robert Richard (Meneja), Masoud Djuma (Kocha Msaidizi), Adel Zrane (Kocha wa Viungo), Mohammed Muharami ‘Shilton’ (Kocha wa Makipa), Yassin Gembe (Daktari) na Yassin Mtambo (Mtunza Vifaa), hivyo Mtathimini wa Mechi atakuwa ofisa wa nane.
Kwa mujibu wa mtandao wa www.coach-logic.com, mtaalam wa tathmini ya mchezo ana majukumu saba ndani ya timu.
Kwanza ni kuitathmini timu pinzani kabla ya mchezo ili kufahamu ubora au udhaifu wao, pili ni kuitathimini mechi mchezo unapokuwa unaendelea. Hapo ataangalia zaidi umiliki wa mpira wa timu yake na wapinzani, ufanisi wa mchezaji mmoja mmoja na pia mbinu za kocha wake na kocha mpinzani.
Baada ya hapo kazi inayofuata ni kurudisha mrejesho kwa benchi la ufundi na wachezaji kwa kile alichokiona na ikiwezekana kushauri nini kifanyike. Jukumu jingine ni kuandaa nyaraka na ripoti kuhusiana na ufanisi wa timu.
Pia mtaalamu anapaswa kutafsiri, kuchambua na kusambaza data zinazohusiana na ufanisi wa timu kwa wachezaji na benchi la ufundi, data ambazo zinakuwa za upande wa timu yake na timu pinzani huku jukumu la sita likiwa ni kusimamia taarifa za ufanisi na maendeleo ya timu.
Mtaalamu huyo atakuwa na jukumu la mwisho ambalo ni kufanya uhariri wa video zitakazotumiwa na benchi la ufundi kabla na baada ya mchezo au mashindano.
MAJUKUMU YAKE:
1. Tathmini ya wapinzani kabla ya mechi
2. Tathmini ya mchezo
3. Kurudisha mrejesho kwa timu
4. Kuandaa nyaraka na repoti za ufanisi wa timu
5. Kutafsiri na uchambuzi wa data
6. Kusimamia taarifa za ufanisi wa timu
7. Kuhariri video
SIMBA DAY
Kaimu rais huyo wa Simba pia alisema klabu yake imejipanga ili kuwa na Simba Day itakayoacha historia kubwa kwa wadau wote.
“Changamoto kubwa ambayo imekuwa ikitukabili ni mauzo ya jezi hasa kwenye siku hiyo. Katika kuhakikisha angalau tunanufaika na mauzo ya jezi zetu, safari hii tumeagiza na tutasimamia wenyewe mauzo ya jezi,” alisema.
“Tumepanga kufungua duka makao makuu ya klabu kwa ajili ya mauzo ya jezi na vitu vingine vyenye nembo ya klabu. Pia siku hiyo ya Simba Day mbali ya utambulisho wa wachezaji wa timu kubwa pia tutawatambulisha wale wa kikosi cha vijana na timu yetu ya wanawake.
“Habari njema kwa Wanasimba ni tumeanza kuiimarisha timu yetu ya wanawake kwa kusajili wachezaji sita mastaa wa timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’. Mkakati wetu ni kuhakikisha tunatwaa ubingwa kwenye mashindano yote tutakayoshiriki upande wa wanawake na wanaume.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.