Azam FC yanasa saini ya Nchimbi

Ditram Nchimbi Azam
Ditram Nchimbi Azam


KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imethibitisha kuingia mkataba wa miaka miwili na mshambuliaji Ditram Nchimbi, akitokea Njombe Mji.

Nchimbi ni mmoja ya washambuliaji wachache kwenye ligi ambao wanatambulika kwa uwezo wa kupambana na mabeki kwa mipira ya juu na chini, akitarajiwa kuongeza kitu katika eneo la ushambuliaji la Azam FC.

Zoezi la uingiaji mkataba baina ya pande hizo mbili limesimamiwa na Meneja wa timu hiyo, Phillip Alando, ambaye ameweka wazi kuwa ujio wa mshambuliaji huyo ni katika kuboresha eneo la ushambuliaji.

Mshambuliaji huyo aliyeipandisha Majimaji miaka mitatu iliyopita kwa mabao yake 10, amewahi pia kuichezea Mbeya City, ataanza kuonekana rasmi Azam FC kuanzia msimu ujao wakati timu hiyo ikianza kutetea ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame inayotarajia kutimua vumbi kuanzia Juni 29 hadi Julai 13 mwaka huu.

Huo ni usajili wa tatu kwa Azam FC kuelekea msimu ujao, awali ikitangulia kuwasajili nyota wawili kutoka Zimbabwe mshambuliaji Donald Ngoma na kiungo Tafadzwa Kutinyu, wote wakipendekezwa na Kocha Mkuu mpya, Hans Van Der Pluijm