watatu wa Mbao FC kuikosa Ndanda


Mbao imevuna pointi 24 na kukaa nafasi ya 14 baada ya kucheza mechi 26, huku Ndanda wakiwa na alama 23 baada ya kushuka uwanjani mara 27.
By Saddam Sadick


Mwanza. Wakati Mbao FC ikitarajia kuwakabili Ndanda kesho kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu, itawakosa nyota wake watatu wa kikosi cha kwanza kutokana na sababu tofauti ikiwamo majeruhi.


Mchezo huo unaotarajia kupigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, utakuwa mkali kutokana na timu zote kuwa katika nafasi mbaya ya kukwepa kushuka daraja.


Hadi sasa Mbao imevuna pointi 24 na kukaa nafasi ya 14 baada ya kucheza mechi 26, huku Ndanda wakiwa na alama 23 baada ya kushuka uwanjani mara 27.


Kocha wa timu hiyo, Novatus Fulgence alisema kuwa nyota wake watatu, beki wa kushoto Aboubakari Mfaume, Kiraka Boniface Maganga na Straika wao Habib Kyombo wataukosa mchezo huo.


Alisema kuwa Mfaume na Maganga wanasumbuliwa na enka,huku Kyombo akiwa na timu ya Taifa ya Vijana (U-20) Ngorongoro Heroes na kwamba amewaandaa mbadala wake.


“Tutawakosa wachezaji watatu wa kikosi cha kwanza kutokana na sababu tofauti, lakini kwa ujumla nimewaandaa mbadala wao na tutafanya vizuri,” alisema Fulgence.


Kocha huyo aliongeza mechi hiyo ni muhimu sana kwao kupata pointi tatu ambazo zitawapa mwanga wa kujinasua na janga la kushuka daraja na kusisitiza kuwa hataki sare wala kupoteza.


“Tunaenda mchezoni kwa tahadhari na umakini mkubwa sana, tunajua Ndanda wakoje, kwa hiyo hatutakubali kupoteza pointi hata moja ili kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo,” alisema kocha huyo.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.