SIMBA SC YAIZIDI KETE CAMEROON KWA PIERRE



NA SAADA SALIM

-BAADA ya Simba kuibanjua Yanga bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, wameamua kuifanyia kauzibe timu ya Taifa ya Cameroon ambayo inaweza kumnasa kocha wao, Pierre Lechantre.

-Mawakala wa Pierre, ambaye aliingia mkataba wa miezi sita na Simba, wametuma maombi nchini Cameroon kwa ajili ya kuomba kibarua hicho cha kuinoa timu hiyo ya taifa, ingawa bado kocha huyo anataka kuhakikisha anaipa timu ubingwa kisha ondoke, jambo ambalo Wekundu wa Msimbazi hawako tayari kuliona likitokea.

-Kocha huyo raia wa Ufaransa, Pierre, ana nafasi kubwa ya kupewa tena kibarua hicho cha kuinoa Cameroon ambayo alishawahi kuifundisha na kunyakua taji la Mataifa ya Afrika mwaka 2000.

-Kocha huyo amelithibitishia BINGWA jana kwamba ni kweli mawakala wake wamepeleka maombi chama cha soka Cameroon, lakini kichwa chake kwa sasa kinaiwaza Simba.

-“Mimi kwa sasa akili yangu ipo kwenye kuisaidia Simba kuhakikisha inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu, hilo suala la kwenda Cameroon tunaweza kulizungumza baadaye,” alisema Pierre.

-Alisema anawapa asilimia kubwa uongozi wa Simba, kulingana na kufikia asilimia kubwa ya makubaliano waliyoingia wakati anasaini mkataba wa kukinoa kikosi cha timu hiyo.

-Wakati Pierre akitajwa kwamba ana nafasi kubwa ya kwenda Cameroon kutokana na rekodi nzuri aliyoiacha huko, taarifa kutoka Simba zinadai kuwa bilionea wao, Mohamed Dewji ‘Mo’, anataka kumwongezea mkataba mrefu.

-Kigogo mmoja aliliambia BINGWA: “Haitakuwa rahisi tumwachie huyo kocha kwani kazi yake ni nzuri na kila mmoja ameiona, hata Mo Dewji (Mohamed Dewji), anataka kukaa naye meza moja kuzungumzia kumwongezea mkataba, kingine yeye mwenyewe pia anaipenda Simba.”

-Simba waliridhia utendaji wake baada ya mchezo wao juzi dhidi ya Yanga na kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo watakuwa wamekamilisha mazungumzo ya kumbakiza katika timu hiyo.

-Kwa sasa Simba inaongoza Ligi Kuu kwa kuwa na pointi 62 baada ya kushuka dimbani mara 26,wakishinda michezo 18 na kutoka sare mara nane wakiwaacha kwa michezo miwili na pointi 14 mahasimu wao Yanga, ambao wanashika nafasi ya tatu.

-Wakati huo huo imedaiwa kuwa kocha huyo, Pierre, amepania kuhakikisha anafikia rekodi ya kocha wa Zambia, Patrick Phiri, ambaye alifanikiwa kuipa ubingwa Simba msimu wa 2009/10 bila kufungwa.
Joseph michael

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.