Domayo amewapa ahadi hii mashabiki msimu ujao

Category: 
Team: 
Azam FC
BAADA ya kumaliza nafasi ya pili msimu huu, kiungo wa Azam FC, Frank Domayo ‘Chumvi’, amewaahidi mashabiki wa timu hiyo kuwa watapambana kuhakikisha wanarejea kwenye michuano ya Kimataifa msimu ujao.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) wameshika nafasi hiyo kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwa na pointi 58, nyuma ya Simba iliyokuwa mabingwa kwa pointi 69 huku Yanga ikimaliza katika nafasi ya tatu kwa pointi zake 52.
Domayo ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa msimu huu ulikuwa mgumu kutokana na timu zote za ligi kuja na ushindani huku akidai wamemaliza katika hatua hiyo waliyofikia kutokana na hali ya kupambana kikosini.
“Msimu ulikuwa mgumu sana kwa sababu kila timu ilijiandaa ilikuwa inapambana kadiri ya uwezo wake kuweza kupata matokeo, kwa hiyo mimi naweza kusema sisi kwa upande wetu tumepata kitu fulani kwa sababu tulikuwa tunajituma, tumefuata maelekezo ya kocha, tumepambana na tumeweza kupata matokeo mazuri kwenye baadhi ya mechi,” alisema.
Watajipanga 2018/2019
Domayo aliyefunga mabao mawili ndani ya mechi tatu za mwisho za ligi na kutoa pasi tatu za mabao, alisema japo hawajafikia malengo ya msimu lakini watajipanga vema kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi msimu ujao.
“Kila timu inakuwa na malengo ya ubingwa kwa sababu ukiwa bingwa unakuwa malengo yako yametimia, naweza kusema sisi malengo yetu hayakutimia lakini pia tumejitahidi kwa sababu tulimaliza msimu wa mwaka jana nafasi ya nne.
“Kwa hiyo msimu huu tumemaliza kidogo nafasi hizi za juu, hivyo tunamshukuru Mungu tumeweza kupambana, kujituma na naweza kusema tunajiandaa kwa ajili ya msimu ujao ili tuweze kufanya vizuri zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Mashabiki waendelee kutusapoti kwa sababu mashabiki ndio wanaotupa morali, moyo uwanjani kwa hiyo watusapoti kadiri ya uwezo wao kwa sababu bila wao sisi hatuwezi tunaonaga hata Ulaya wanacheza na mashabiki wengi uwanjani ili kushangilia na kusapoti timu.
“Waendelee kutusapoti wasikate tamaa na sisi tunawaahidi hatutawaangusha msimu unaokuja, tutapambana kuweza kupata nafasi nzuri zaidi ya kuwakilisha nchi Kimataifa.”
Mafanikio binafsi
Akizungumzia siri ya kiwango chake bora msimu huu, Domayo aliyefunga mabao matatu kwenye mashindano yote msimu huu, alisema kwa kiasi kikubwa yametokana na hali ya kujituma, kufanya mazoezi na kufuata maelekezo ya kocha.
“Kwa sababu ukijituma, ukifanya mazoezi na ukifuata maelekezo ya kocha unapambana kadiri ya uwezo wako ili uweze kutetea namba, naweza kusema timu yetu ina wachezaji wengi na wazuri, kwa hiyo kujituma kwako na kufuata maelekezo ya kocha kunaweza kukupa mafanikio ya kuweza kucheza kwenye hiki kikosi,” alisema

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.