ALIYESHANGILIA BAO AKIWA NA ‘RED CARD’ AFUNGIWA MECHI TATU



Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia mechi tatu na kumpiga faini ya shilingi laki tano mchezaji wa Mbeya City Ramadhan Malima kwa kosa la kuingia kushangilia goli la timu yake wakati akiwa tayari ameoneshwa kadi nyekundu.

Uamuzi huo umetangazwa leo na kamati hiyo iliyokutana Mei 9, 2018 ambapo pamoja na mambo mengine ilipitia mashauri manne yaliyofikishwa kwenye kamati, mojawapo likiwa linamuhusu mchezaji huyo.

Mchezo huo uliopigwa Aprili 22 kwenye dimba la Sokoine jijini Mbeya, ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Taarifa hiyo imeeleza pia kuwa mashauri mengine kadhaa hayakusikilizwa baada ya kutofika kwa washtakiwa wa mashauri hayo na kamati imeomba wapewe wito wa mwisho ambao kama hawatafika kamati itasikiliza mashauri yao katika upande mmoja na kuyatolea uamuzi.

Miongoni mwa ambao hawakufika ni Aristica Cioaba (Kocha wa Azam FC) na Kelvin Yondan (Mchezaji wa Yanga) wakati ikielezwa kuwa Meneja wa Singida United Ibrahim Mohamed alitoa taarifa ya kufiwa na baba yake mzazi.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.