Ajib Awatolea Uvivu Mashabiki Yanga

Kiungo mshambuliaji wa timu ya Yanga amewatolea uvivu mashabiki waliodhani alifanya makusudi kutosafiri na kikosi hicho kwenda Algeria kwa ajili ya mchezo wa kwanza dhidi ya USM Alger leo.

Mchana wa jana Ajibu amefanikiwa kupata mtoto wa kike kufuatia mke wake kujifungua katika ujauzito ambao ulikuwa na matatizo.

Ajibu amesikitishwa na watu waliomtumia ujumbe kumtuhumu kutosafiri na timu kwenda Algeria kwa sababu ya kudai mshahara wake.

"Namshukuru Mungu kwa kutujalia kupata mtoto wa kike, hapo kabla kulikuwa na hofu kubwa sababu ujauzito wake ulikuwa na matatizo mengi. Kuna wakati nilikuwa na hofu kubwa juu ya maisha yake.

"Naumizwa na wanaonishambulia kupitia sms kuwa nimegoma kuichezea timu, sina sababu ya kufanya hivyo mpira ni kazi yangu.

 "Nawasamehe kwa sababu wangesikia mke wangu amefariki kwa matatizo ya uzazi nadhani wangesema mengine," aliandika Ajibu.

Ajibu ni miongoni mwa nyota wa kikosi cha kwanza walioshindwa kusafiri na timu kutokana na sababu mbalimbali.

Wachezaji wengine wa Yanga walioshindwa kusafiri na timu ni Nadir Haroub, Kelvin Yondani,  Thaban Kamusoko, Obrey Chirwa na Papy Tshishimbi.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.