KAMA TFF WANAAMINI MAANDALIZI NI KUPANGA VIINGILIO, SI AJABU NGORONGORO KUBANWA NYUMBANI


BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
WIKI iliyoanza vizuri kisoka nchini Tanzania baada ya ushindi wa mabao 2-0 wa timu ya taifa ya wakubwa dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inahitimishwa kinyonge baada ya mechi baina ya vijana chini ya umri wa miaka 20 wa nchi hizo mbili jana.
Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes imejiweka pagumu katika kinyang’anyiro cha tiketi ya Fainali za vijana wa umri Afrika mwakani nchini Niger baada ya sare ya 0-0 DRC jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa sare hiyo, Ngorongoro inayofundishwa na kocha Ammy Ninje anayesaidiwa na Juma Mgunda, Boniface Pawasa katika mazoezi ya nguvu, Meneja Leopold Mukebezi ‘Tassle’ na kicha wa makipa, Saleh Machuppa italazimika kwenda kushinda ugenini wiki mbili zijazo kwenye mchezo wa marudiano.

Serengeti haikuwa na bahati tu kwenye mchezo huo, kwani ilitengeneza nafasi nzuri za kufunga zaidi ya sita, lakini ugumu ulikuwa kwenye umaliziaji na sana kutokana na umahiri wa safu ya ulinzi ya wachezaji wa DRC wenye miili mikubwa.
Jumanne wiki hii Taifa Stars iliifunga DRC 2-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Shiza Ramadhani Kichuya wa Simba ya nyumbani.
Huo ulikuwa ushindi wa kwanza Tanzania tangu Julai 7 mwaka jana ilipoichapa kwa matuta Lesotho baada ya sare ya 0-0 kwenye Kombe la COSAFA mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
Tanzania iliingia kwenye mchezo wa leo ikitoka kufungwa 4-1 na Algeria mjini Algiers Machi 22 katika mchezo mwingine wa kirafiki na kwa ujumla huu ni ushindi wa kwanza kwa Taifa Stars ndani ya mechi 10, ikifungwa nne na sare tano.
Taifa Stars ilitoa sare mbili mfululizo na Rwanda kufuzu Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), 1-1 Julai 15 mjini Mwanza na 0-0 Julai 22 mjini Kigali, kabla ya kutoa sare nyingine za 1-1 mfululizo na Malawi mjini Dar es salaam Oktoba 7 na Benin Novemba 12.
Ikatoa sare ya 0-0 na Libya Desemba 3, ikafungwa 2-1 mara mbili, kwanza na Zanzibar Desemba 7, baadaye na Rwanda Desemba 9 na 1-0 na Kenya Desemba 11 kwenye michuano ya Challenge mjini Nairobi.
Na kwa Ngorongoro ilitoa sare na DRC baada ya kushinda mechi mbili mfululizo za kirafiki, kwanza 1-0 dhidi ya Morocco na baadaye 2-1 dhidi ya Msumbiji.
Matokeo ya mchezo huo yanamaanisha kwamba kuna sehemu kulikuwa kuna mapungufu katika maandalizi ya timu.
Maandalizi si kambi ya mazoezi pekee, kuna vitu vingi vinahusika ikiwemo kuwatayarisha vijana kisaikolojia kuelekea mchezo husika, ili wajue tofauti ya kuingia kwenye mchezo wa kirafiki na mchezo wa mashindano.
Tanzania siku zote tumekuwa tuna makosa ya aina ile ile ukiondoa mapungufu yetu ya asili, kwamba hatujui kutofautisha mambo na tunachukulia kila kitu ni sawa – kwamba mechi ya kirafiki na ya mashindano ni sawa na unavyocheza na mpinzani huyu, unaweza kucheza na mpinzani yeyote.
Viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wao wanaamini kwa upande wakishapanga viingilio na walinzi magetini wamemaliza, lakini kumbe kama ‘baba’ wa soka ya nchi wana majukumu zaidi ya hayo katika kufanikisha ustawi wa mchezo.
Nilichokiona kwenye mchezo baina ya Ngorongoro na DRC ni kuuchukulia kama wa kawaida, kumbe ilikuwa mechi ya mashindano ambayo tulihitaji kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri kuelekea mchezo wa marudiano.
Sasa tumejibebesha mzigo wa kwenda kupigania ushindi wa ugenini lazima au sare ya mabao ili kusonga mbele, tu kwa kukosa mipango ya kushinda nyumbani.

Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.