Wakili wa Wambura, alaani uteuzi wa Nyamlani



Wakili wa aliyekuwa Makamu Rais wa shirikisho la soka nchini (TFF) Michael Richard Wambura, ndugu Emmanuel Muga Augustino amesema anashangazwa na kamati tendaji kumteua Athuman Nyamlani kuwa Kaimu Makamu Rais wa TFF wakati ambapo bado rufaa ya mteja wake bado haijasikilizwa.

Wakili Muga amesema Wambura ambaye tayari amekata rufaa kupinga hukumu ya kufungiwa maisha kutokana na tuhuma za kutumia ofisi vibaya, amelaani ukiukwaji wa katiba ya TFF kumteua Nyamlani na ameitaka Serikali kuingilia kati kukomesha kitendo hicho alichokitaja kama mchezo mchafu.

“Kamati tendaji ya TFF imemteua Athuman Nyamlani kuwa kaimu makamu wa Rais, kinyume na Ibara ya 34 ya Katiba ya TFF ambayo haitoi mamlaka ya uteuzi kwa kamati tendaji, kwa uteuzi huo kamati ya utendaji imevunja ibara ya 34(1) a,b,c,d,e,f,g,h,I,j,k,l,m,n,o,p na q ya katiba ya TFF Tolea la 2015,” Muga amesema.

Aidha Muga amesema mteja wake amelalamikia kitendo cha Kamati Tendaji kufanya mabadiliko katika kamati ya maadili ya Rufaa ya TFF ambayo ndio ilipaswa kusikiliza rufaa ya mteja wake aliyoiwasilisha Jumamosi ya Machi 18, 2018.

“Kamati Tendaji pia imebadilisha wajumbe wa kamati ya maadili ya Rufaa ya TFF na kuweka watu wapya wakati tayari Michael Wambura ameshakata rufaa, kwa mabadiliko hayo TFF imevunja ibara ya 34 (2), (Vyombo vya kutoa haki vya TFF ni huru na wajumbe wake hawataondolewa kabla ya kumaliza muda wao bila idhini ya mkutano mkuu) ya katiba ya TFF,” Muga ameongeza.

Muga ameeleza kuwa hiyo ni dalili tosha ambayo inaonesha kuwa TFF kwa maksudi imedhamiria kukiuka katiba ili kudidimiza haki ya Michael Wambura.

“Wambura alifungiwa bila kusikilizwa na kamati isiyo na mamlaka na baada ya kukata rufaa kwa hati ya dharura, rufaa yake imecheleweshwa kwa maksudi wakati wajumbe wote wapo Dar es Salaam, ukiondoa mmoja,” Muga amelalama.

Kwa mujibu wa wakili Muga, ni kuwa Michael Wambura ameiomba serikali kupitia baraza la michezo la Taifa kuingilia mara moja kuzuia ukiukwaji wa katiba na sheria na iwaelekeze TFF waitishe kikao cha rufaa bila mabadiliko yoyote ili haki itendeke.

Amefungiwa maisha



Ikumbukwe kuwa mchana wa Machi 15, 2018 Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), imemfungia maisha kutojihusisha na shughuli za soka Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura.



Inadaiwa kuwa Wambura amefungiwa kutokana na kupokea fedha zisizo halali kiasi cha Shilingi milioni 84, pamoja kughushi nyaraka za malipo, na kula njama kulipwa fedha na waliokua viongozi wa TFF Jamal Malinzi na Selestin.

Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.