Nyosso Amaliza Adhabu, Rasmi Kurejea Kikosini Kagera
Mara baada ya kitendo cha utovu wa nidhamu na kuadhibiwa Mlinzi wa kati wa Kagera Sugar, Juma Nyosso amerejea katika kikosi hicho baada ya kumaliza adhabu yake tayari kuivaa Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa Aprili 8 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Nyosso amemaliza adhabu yake ya mechi tano aliyokuwa akitumikia kwa kumpiga shabiki baada ya mechi kati ya Kagera Sugar dhidi ya Simba.
Kocha Msaidizi wa Kagera, Ally Jangalu alisema wamejipanga kikamilifu kuwakabili Ndanda na vijana wameimarika hasa baada ya Nyosso kuwa huru.
Kocha Jangalu alisema watamkosa beki Mohamed Fakhi mwenye kadi tatu za njano na kwamba hawana wasiwasi isipokuwa wanahitaji pointi tatu.
“Tunaendelea kujifua zaidi na vijana wanaimarika kila siku, tumeazimia kupata pointi tatu na Nyosso (Juma) amemaliza adhabu yake hivyo uwenda akawemo kikosini,” alisema Jangalu.
Kocha huyo aliongeza kuwa kwa kipindi hiki ligi imesimama, wamejikita zaidi katika kuwajenga wachezaji fiziki, kiakili, kisaikolojia na kiushindani ili mchezo dhidi ya Ndanda waanze kuhesabu pointi.
Alisema kuwa wanaamini mpambano huo kuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kuhitaji ushindi ili kujiweka nafasi nzuri,hivyo watawavaa kwa tahadhari kubwa.
Kagera Sugar imekusanya pointi 21, ikiwa nafasi ya 12, huku Ndanda wakiwa na alama 22 katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kucheza mechi 22 kwa timu hizo.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.