Ndairagije atoa somo, mchakato wa kumpata Kocha mpya Taifa Stars


Kocha mkuu wa timu ya soka ya Mbao ya Mwanza, Etienne Ndairagije ametoa ushauri mdogo kwa shirikisho la soka nchini (TFF) katika kipindi hiki ambacho wanatafuta kocha mpya wa timu ya Taifa.

Ndairagije amesema TFF kupitia kwa mkurugenzi wao wa ufundi (Salumu Madadi) wanatakiwa kufanya utafiti mdogo wa aina ya wachezaji walionao ili kujua aina ya mchezo watakaouchagua kabla ya kumleta Kocha.

"Tanzania inatakiwa kufanya utafiti wa wachezaji wake, je wanamaumbo makubwa? Kama ndivyo basi wacheze aina ya gani ya mpira, kama wanamaumbo madogo basi wachague aina gani kama ni mfumo wa kuweka chini mpira, lakini pia wanaweza kutumia tik taka style Kama wachezaji wao wana ufundi," Ndairagije amesema.

Kocha huyo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kwa kuisaidia timu dhaifu ya Mbao kuwa na mafanikio ya haraka, amesema ni jambo la kushangaza kutarajia kocha ataleta mafanikio makubwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa bila TFF wenyewe kuwa na mipango ya awali ya kulitengeneza soka lenyewe.

"Kocha ni kama mjenzi ambaye anategemea ramani kutoka kwa mwenye nyumba, anajenga nyumba kutokana na ramani ya awali, huwezi kutegemea kocha akakipa mafanikio kikosi chako bila kumpa mpango mkakati, au philosophy of playing, hilo ndo jambo la msingi," ameongeza.

Aidha kocha huyo ameonesha kukasirishwa na hatua ya mchezaji Habibu Haji Kiyombo kutoitwa katika timu yoyote ya Taifa wakati ana kiwango kizuri na bado kijana.

"Ujue Habibu bado hata miaka 19 bado hajafika, Sina shida na kutoitwa kwake Taifa Stars lakini alipaswa kuitwa timu ya vijana ya Ngorongoro Heroes, huo ndio ukuaji wa wachezaji katika timu za Taifa, sasa kumuacha Habibu ni jambo ambalo hata mimi bado silielewi," amesema.


Ukocha sio CV

Akizungumza na kipindi cha michezo na Burudani wiki hii kinachorushwa na Radio Free Africa, Ndairagije amesema kocha haajiriwi kwa CV aliyonayo bali makubaliano maalumu na waajiri wake kutokana na mipango ambayo wanakuwa wanawekeana katika utiliwaji saini wa mkataba.

Tanzania ipo katika mchakato wa kutafuta mrithi wa kocha Salumu Shabani Mayanga ambaye mkataba wake umemalizika toka mwanzoni mwa mwaka huu.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.