Mayanga akanusha taarifa za kumsakizia Moroko, kipigo cha Algeria
Kocha mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Salumu Shaban Mayanga, amekanusha taarifa zilizozagaa mitandaoni kuwa amemtupia mzigo wa lawama kocha Msaidizi Hemedi Suleiman (Moroko) kutokana na kufanya vibaya katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Algeria.
Mayanga amesema taarifa hizo hazina lengo zuri, kwani zina nia ya kuwavuruga Watanzania na ni upotoshaji mkubwa ambao katu haupaswi kufumbiwa macho kwa namna yoyote ile.
"Taarifa inayozunguka mitandaoni kuwa sichagua timu ya Taifa siyo sahihi, ni upotoshaji wenye nia ya kutuvuruga, watu waache kuupotosha umma, mimi ndiyo nimechagua kikosi chote kilichosafiri kwenda Algeria na si mwingine, kocha Hemed Morocco nilimuachia jukumu la kukitangaza baada ya uteuzi" amesema Mayanga.
Taarifa zilizogaa zilisema kwamba Mayanga akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Algeria alisema kuwa hakuwepo kwenye uteuzi wa kikosi hicho, ambacho asilimia kubwa ya wachezaji walikuwa hawana fitness ya mchezo.
“Kumekua na maneno mengi kuhusu hiki kikosi cha timu ya Taifa kwanza mimi sikuwepo wakati kikosi kinateuliwa aliyeteua ni kocha msaidizi, pamoja na kamati ya ufundi ya TFF mimi nilikuwa nje nimekuja nimekuta kikosi tayari kimetangazwa,” Taarifa hiyo ilimnukuu kocha Mayanga.
Kipigo cha mabao 4-1
Katika mchezo huo ambao ulifanyika Machi 22 mabao ya Algeria yalifungwa na Baghdad Bounedjah mawili dakika ya 12 na 79, Shomari Kapombe moja aliyejifunga dakika ya 45 katika harakati za kuokoa na Carl Medjani dakika ya 53, wakati la Tanzania lilifungwa na Simon Msuva dakika ya 20.
Huo ulikuwa ni mwendelezo wa ubabe wa Algeria kwa Tanzania baada ya Novemba 17, mwaka 2015 The Green kuichapa 7-0 Taifa Stars katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia Uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.