Kunambi awaita vijana kujizolea mikopo
Kunambi alisema hayo juzi, wakati alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini hapo.
Alisema kuwa mpaka sasa katika mfuko wa kuwakopesha vijana, kinamama na watu wenye ulemavu una kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 1.7, lakini hakuna vikundi ambavyo vinajitokeza kukopa hata kimoja.
Alisema kuwa fedha hizo bado zipo changamoto iliyopo ni kwa vijana, watu wenye ulemavu na kinamama wamekuwa wakitumia muda mwingi kukaa kwenye makundi bila kuwa na shughuli yoyote ya uzalishaji na badala yake wanalalamika kwa madai kuwa maisha ni magumu.
Kunambi, alisema kuwa kutokana na jiji kuwa na mapato makubwa kwa hivi sasa kuna fedha za kutosha ambazo vijana, kinamama na watu wenye ulemavu wanaweza kujiunga kwenye vikundi na wakapatiwa mikopo hiyo.
“Ninaomba nitumie nafasi hii kwa kupitia vyombo vya habari kwa kuwaambia watu wenye ulemavu vijana na kinamama waungane kwa pamoja kwa kuanzisha vikundi ili waweze kuomba mkopo kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kimaisha," alisema.
Alisema kuwa kwa hivi sasa hakuna sababu ya makundi hayo kukaa bila kujishughulisha na kulalamika kutokana na hali ngumu ya kimaisha wakati kuna fursa za kutosha kwa upande wa jiji kwa sasa kuna fedha zaidi ya Sh. bilioni 1.7.
Katika hatua nyingine mkurugenzi huyo amewaonya vijana na kuwataka kuachana na tabia ya kulalamika kutokana na ukosefu wa kazi ndani ya jiji, badala yake watumie fursa za uwekezaji ikiwamo ujenzi wa miondombinu mbalimbali inayoendelea kwa hivi sasa.
Alisema kuwa kwa sasa Jiji la Dodoma lina shughuli mbalimbali nyingi ikiwamo za ujenzi wa mji wa kiserikali, ujenzi wa stendi kuu ya mabasi pamoja na ujenzi wa treni ya mwendo kasi, hivyo hakuna sababu ya kuinyooshea serikali vidole kuwa hakuna kazi.
“Unaweza kutumia nguvu yako kufanya kazi kwa kujipatia kipato, lakini kama unaujuzi unaweza kutumia ujuzi wako kwa ajili ya kujiongezea kipato kwa kuwa siamini kama ukiamka asubuhi ukaanza kuzungukia kwenye sehemu za ujenzi zinazoendelea kujengwa kama utakosa kazi ya kufanya.
Alisema kuwa kwa hivi sasa Mkoa wa Dodoma unafursa nyingi za kufanya kutokana na shughuli zinazofanyika ikiwamo ujenzi wa ofisi za wizara zinazojengwa ambazo zinahitajika watumishi wake wahamie Dodoma.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.