Zahera: Wachezaji wa Tanzania hawajitambui


Kocha wa timu ya Taifa ya Congo na Yanga, Mwinyi Zahera amekizungumzia kitendo cha wanasoka wa Tanzania, kushindwa kutii wito wa kocha wao wa taifa, Emmanuel Amunike kwamba ni ishara ya kutojitambua.

Zahera alisema katika timu ya taifa ya Congo mchezaji akichelewa dakika tano ya mazoezi anakatwa dola 500 na klabu yake anayoichezea Ligi Kuu na akichelewa dakika 10 ni dola 1500.

"Congo wamejiwekea misingi imara ya ushirikiano unaanzia kwa makocha wa klabu na viongozi wao kuhakikisha mchezaji anapotoka kwenye timu yao anakuwa mfano wa kuigwa kwa nidhamu na kiwango chake hasa kwa kupata namba ndani ya kikosi cha kwanza.

"Hivyo mchezaji anapokuwa anachelewa mazoezini ama anaonyesha utovu wa nidhamu mimi kocha wa timu ya taifa naandika ripoti yake kwenda kwa viongozi wake wa klabu ambao ndio wanachukua hatua ya kumuwajibisha kwa makosa yake, hilo nimeliona limesaidia kwa hali ya juu sana na kila mchezaji anakuwa na hamu ya kuitwa kulitumikia taifa lake, tofauti na Tanzania wanaojivuta vuta na kuona wao wapo juu ya taifa, hii ni mbaya sana,"alisema Zahera.

Alistajabishwa na kile kilichotokea kwa wachezaji ambao wameanguliwa kwenye mpango wa kikosi cha kocha Amunike,  kwamba kama wanashindwa kuwa na moyo wa uzalendo na taifa lao ni dhahiri kwamba hawaangalii mbali na kujiona wamemaliza kila kitu.

"Asilimia kubwa ya wachezaji wa Tanzania wameshindwa kuishi kwa kuzingatia taaluma yao, hasa nimeona kama wanapenda sifa kuliko kuwajibika, kocha Amunike ni mtu anayejua mpira kwani amecheza katika mataifa yalioendelea, analolifanya liwafunze na wengine, lasivyo wataishia kucheza ligi hiyo hiyo," alisema Mkongo huyo.

Pamoja na kwamba wameanguliwa kwenye mpango wa Amunike, kocha Zahera aliwashauri wachezaji hao kuiomba radhi nchini yao na kujutia kile ambacho wamekifanya, akisisitiza kinakinzana na taluma yao ya mpira wa miguu Duniani.

"Kwanza wachezaji ndio wanaopaswa kuwa na uchungu na maendeleo ya nchi yao, wawe waungwana waombe radhi, pia waige mfano wa wachezaji wa Ulaya ambao wanayatumikia mataifa yao kwa moyo wa uzalendo," alisema Zahera.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.