KOCHA YANGA ,NILETEENI KOCHA WA SIMBA DJUMA YANGA

Djuma-sokakiganjani

YANGA wanafikiria kumpa ofa Kocha mwenye mbwembwe mazoezini, Masoud Djuma kama Simba wakikubaliana kumpiga chini.

Lakini Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera ambaye mpaka sasa hana msaidizi, jana Jumamosi akiwa Liberia amezungumza na Spoti Xtra na kusema anamjua Djuma na akiletewa atapiga nae mzigo freshi kwa vile ni mzoefu.

Habari za ndani ya Simba zinasema kwamba uongozi uko kwenye mchakato wa kumuondoa Djuma kwa kile kilichoelezwa kwamba picha haziivi na bosi wake, Mbelgiji Patrick Aussems ambaye inadaiwa amewabonyeza viongozi wampige chini.

“Sina tatizo lolote kikubwa ni kufuata utaratibu tu wa kazi ambao yeye kama kocha anaujua, kwa hiyo kama itatokea ikawa hivyo mimi sina tatizo nitafanya naye kazi,” alisema Zahera ambaye Msaidizi wake, Shadrack Nsajigwa alijiuzuru kukwepa presha na lawama za mashabiki.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba baadhi ya viongozi wameanza kujadiliana uwezekano wa kumpa ofa kocha huyo ingawa wengine wanapinga, licha ya kwamba Haji Manara amekuwa akisisitiza kwamba Djuma haondoki.

Wanaopendekeza achukuliwe wanadai kwamba Djuma ana uwezo wa kujenga morali na ndiye anayefanya kazi kubwa ndani ya Simba kwa sasa licha ya wengi kumuangalia Mbelgiji.

Lakini vigogo wengine ndani ya Yanga wanaopinga waziwazi wazo hilo wanadai kwamba Kocha huyo ana Usimba na ameshatengeneza mtandao mkubwa Msimbazi hivyo itakuwa ngumu kufanya kazi kwa moyo Yanga.

Lakini Mwenyekiti wa Kamati ya usajili wa Yanga, Hussein Nyika alipoulizwa kuhusiana na ishu hiyo jana alizuga na kusisitiza kwamba bado wanaendelea na mchakato wa kutafuta msaidizi wa Zahera.

Djuma jana hakutoa ushirikiano kuhusiana na hatma yake ndani ya Simba lakini Spoti Xtra lilidokezwa kwamba jioni alikuwa na kikao na baadhi ya vigogo wa Msimbazi ambacho moja ya vitu ni kuzungumzia ishu ya kumpiga chini.

Lakini mjadala huenda ukaibuka kwenye ishu ya mkwanja kwani Djuma kwa sasa analipwa Sh.Mil.13.6 Simba akiwa kama Kocha Msaidizi ambazo ni nyingi kuliko Zahera ambaye Yanga wanamlipa Sh.Mil.6.8.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.