Ligi yamtoa jasho Mbelgiji Simba SC


. Licha ya kupata pointi sita katika mechi mbili, kocha wa Simba Patrick Aussems, amekiri Ligi Kuu Tanzania Bara ni Ligi yenye ushindani mkubwa.
Aussems, alitoa kauli hiyo juzi muda mfupi baada ya Simba kuilaza Mbeya City mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili, kocha huyo alisema amebaini ligi ina ushindani mkubwa baada ya kupata ushindi kwa mbinde katika mechi mbili ilizocheza Simba msimu huu.
Awali, Simba ilipata ushindi mwembamba katika mchezo wa ufunguzi ilipoilaza Prisons bao 1-0. Mshambuliaji Meddie Kagere amefunga mabao yote matatu.
Alisema timu zote zimeonyesha ushindani na kila moja inapambana kupata pointi tatu katika mchezo husika.
“Ligi ni ngumu hakuna timu inayotaka kupoteza mchezo, tunapambana lengo ni kuhakikisha tunaendelea kupata ushindi kama tulivyoanza, matokeo mazuri kwa kila mchezo yatatuweka sehemu nzuri kwenye Ligi Kuu,”alisema Aussems.
Ausseums alisema anaamini wachezaji wake katika kila idara wataongeza kasi ili kupata ushindi katika mechi zao kwa kuwa mkakati wao ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.
Kocha wa Mbeya City, Ramadhani Nswazurwimo, alidai licha ya kufungwa, vijana wake walicheza kwa nguvu na walipambana dakika zote 90 kutaka ushindi lakini hawakuwa na bahati. “Simba ni timu bora unapocheza nayo unatumia mbinu tofauti, walituzidi katika mchezo kutokana na uzoefu wao tunaangalia mechi zetu zijayo,” alisema kocha huyo.
Matokeo ya juzi yamepunguza presha kwa Aussems ambaye alianza kuingia katika mtego wa baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo baada ya Simba kucheza chini ya kiwango katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Prisons ingawa walishinda.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.