Kambi ya Azam FC Uganda usipime



KAZI KAZI! Ndio unavyoweza kuielezea kambi ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, hapa nchini Uganda, kutokana na maandalizi makali wanayofanya ikiwa ni siku ya pili tokea iwasili nchini humo.

Msafara wa Azam FC umetua jana mchana nchini humo na kujichimbia katika Hoteli ya Top Five, iliyopo Ntinda, jijini Kampala, wakiweka kambi ya wiki mbili itakayoambatana na takribani mechi nne hadi tano za kirafiki kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam Agosti 16 mwaka huu.

Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi, limeonekana kujipanga kuiandaa vema timu hiyo kutokana na mazoezi makali ya kutafuta ufiti wanayoendelea kufanya, wakianza jana jioni na leo Jumanne asubuhi.

Wachezaji wote wamejumuika kwenye programu hiyo, isipokuwa winga Joseph Kimwaga na mshambuliaji Donald Ngoma, wanaofanya programu ya mazoezi mepesi na Nahodha Mkuu Agrey Moris, aliyepewa mapumziko ya siku kadhaa kutokana na kuwa mgonjwa.

Akiongea na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kwa niaba ya wachezaji wenzake, Nahodha Msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi’, alielezea kufurahishwa na mazingira ya kambi kiujumla huku akiwaambia mashabiki wa timu hiyo watajiandaa vema kwa ajili ya kuonyesha ushindani msimu ujao.

“Kwanza tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufika salama Uganda, tunajiandaa vizuri kwa sababu tunafuata maelekezo ya kocha, programu nzuri, tunakaa Hoteli nzuri kumetulia, ni jambo la kila mchezaji kujiandaa vizuri, kuonyesha jitihada mazoezini mwisho wa siku tuweze kupata matokeo mazuri msimu ujao,” alisema.

Matarajio makubwa ya Azam FC kwenye ziara hii wanayoifanya kwa mara ya tatu, ni kukiandaa vema kikosi hicho kiufundi na kimwili ili kuweza kukabiliana na ushindani kuelekea msimu ujao 2018-2019 na kutwaa makombe kama ilivyofanya mwezi uliopita ilipotwaa kwa mara ya pili mfululizo michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup).

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.