UCHAMBUZI WA MECHI YA WATANI WA JADI KESHO SIMBA DHIDI YA YANGA SC


Mchezo wa kesho wa watani wa jadi Simba SC na Yanga SC huenda ndio ikawa mechi ya kuamua bingwa wa ligi kuu msimu huu wa 2017-18 kutokana na msimamo wa ligi ulivyo . Simba wapo kileleni mwa mwa msimamo huo wakiwa na alama 59 huku Yanga akishika nafasi ya pili kwa alama 48.

Simba wamecheza mechi 25 huku Yanga wakicheza mechi 23 kabla ya mchezo wa kesho. Endapo Simba atashinda mchezo wa kesho atafikisha alama 62 akiwa na michezo 26 akibakiwa na michezo 4 mkononi ambayo akishinda michezo yote atafikisha alama 72 huku Yanga akifungwa kesho akiwa ametimiza michezo 24 na kubakiwa na michezo sita ambayo hata akishinda yote atafikisha alama 66 pungufu ya alama 6 kwa Simba SC.

Kisoka ni hesabu ngumu na zinaweza kugeuka wakati wowote endapo mmoja wao akapotea katika malengo yake. Ukali wa hesabu hizi kunaifanya mechi ya kesho kuwa ngumu na yenye pressure kubwa kwa timu zote mbili na kuipa hadhi halisi ya mechi ya watani wa jadi namba tatu kwa umaarufu Afrika baada ya Al Ahly vs Zamaleki na Kaizer Chiefs vs Orlando Pirates.

SIMBA SC

Ni dhahiri wana kiu ya kuunyakua ubingwa wa msimu huu wakiwa na rekodi nzuri ya kutopoteza mchezo hata mmoja . Tayari wamecheza mechi 25 bila kufungwa wakiwa na kipa wao mahiri langoni Aishi Manula ambaye katika michezo hiyo 25 ana ‘ clean sheets ‘ 18 akiwa golikipa pekee kufanya hivyo msimu huu wa ligi kuu. Mfaransa Lanchantre si jambo la kusita kumtumia kesho kama mlinda mlango namba moja dhidi ya Yanga.

Yusufu Mlipili ni chaguo jingine la Lachantre kwenye kikosi cha kesho. Sioni sababu ya kumuanzishia nje akiwa yupo vyema kutokana na ubora wake wa hivi karibuni. Licha ya kuchezeshwa kama mlinzi lakini amekuwa na msaada mkubwa eneo la kiungo cha chini kutokana na determination yake kimbinu. Uwezo wa kukaba na pass zake ndefu huleta muunganiko mzuri kimbinu na safu ya ushambuliaji.

Sambamba na Mlipili pia yupo Shomari Kapombe ambaye toka atoke kwenye majeraha amekuwa mwiba mkali kwa wapinzani wa Simba SC . Amegeuka kiraka kuzimudu nafasi nyingi uwanjani kitu ambacho hivi karibuni benchi la ufundi la Simba SC wameanza kumtumia kama kiungo wa juu. Kiufundi hapa, Simba inatumia 3-5-2 mfumo ambao unahitaji uwe na idadi nzuri ya viungo wakabaji wenye uwezo wa kukaba pia kuchezesha timu ili walinzi watatu nyuma wasizidiwe pia washambuliaji juu wawe na njia nyingi za kuwapatia mipira. Kapombe anaifanya vyema hii kazi hivyo Yanga wawe nae macho.

Asante Kwasi ndio mlinzi pekee wa kati ligi kuu mwenye goli 7 kwenye msimamo wa wafungaji ligi kuu. Kwasi ana uwezo wa kucheza kati au pembeni na toka aingie Simba ameweza kuchukua nafasi ya Mohamedi Hussein upande wa kushoto . Hii inatokana na ubora wake wa kukaba, kukaa na mpira , kutawanya pia kupiga faulo hivyo naamini kesho washambuliaji wa Yanga kati au pembeni watakutana na mlinzi huyu.

Silaha kubwa ya Simba ukiondoa ubora wa safu yao ya ulinzi , ni jinsi ambavyo kiungo chao kinavyocheza hivi sasa. Ndani ya 3-5-2 au 4-4-2 wakiwa na ‘ diamond midfield ‘ kwa maana ya uwepo wa James Kotei kiungo cha chini , Shiza Kichuya kushoto au kulia , Erasto Nyoni , Yusufu Mlipili na Shomari Kapombe au Mzamiru Yassin; hawa wote wana vitu viwili vya kushabihana . Kwanza wote wana uwezo mzuri kukaba pia wana uwezo wa kucheza timu ( double pivot ). Hii inawafanya Simba kuwezo kutawala eneo la kiungo pia kuwa na uwezo wa kuingia kwenye 18 yards ya timu pinzani  kwa njia zote tatu yaani kulia , kushoto na kati. Hawa wote wanaunganishwa na Emanuel Okwi ambaye kuna wakati hucheza kama ‘ play maker ‘ kuunganisha kazi za viungo na mawinga ili John Bocco na invisible attacking midfielder yeyote kutokana na mbinu za mwalimu wawe na fursa nzuri kufunga au kutengeneza faulo kimbinu.

Hivyo Yanga kesho ni lazima wawe makini na patterns za Simba SC hususani eneo la kati na kwenye wings.

YANGA SC

Ni moja ya mechi ambayo inakwenda uwanjani ikiwa na tahadhari kubwa kutopoteza mchezo huo kwa maana ya kusimama kama njia panda kwao ya mafanikio msimu huu kwa soka la ndani. Mapema mwaka huu walishindwa kunyakua kikombe cha Mapinduzi kule Zanzibar pia kutolewa hatua ya robo fainali kombe la ASFC. Mechi ya kesho ni karata ya turufu kuamua ubora wao kwa soka la ndani kwa maana ya kujiweka nafasi nzuri ya kutetea ubingws wao wa ligi kuu .

Kama ilivyo kwa Simba SC ambaye alitoka sare ya 1-1 mchezo wao wa mwisho la Lipuli FC pia Yanga wanakwenda kuivaa Simba SC kesho wakiwa wana kumbukumbu ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City.

Zahera Mwinyi kocha mpya wa Yanga ambaye hii huenda ikawa mechi yake ya kwanza endapo taratibu za kupata kibali cha kufanya kazi nchini atakuwa amepata, ni dhahiri atawategemea Shadrack Nsajigwa na Noel Mwandila wasaidizi wake ambao wamekuwa na timu hiyo kwa muda mrefu katika upangaji wa timu na kumjulisha ubora na udhaifu wa wapinzani wao.

Ni dhahiri langoni atasimama Youthe Rostand na benchi atakuwepo kijana Ramadhani Kabwili hii ni kutokana na kujitonesha kwa golikipa namba mbili wa timu hiyo Beno Kakolanya mazoezini Morogoro.

Ubora wa Simba SC eneo la kati na kwenye wings utawafanya Yanga kukuna vichwa wachezaji gani ambao itawapanga eneo la kati na pembeni ili kuzuia mtiririko wa Simba kuanzia nyuma kuja juu.

Papy Tshishimbi ni bora eneo la kiungo cha chini lakini hali yake yakuwa majeruhi inatia shaka kuwamudu vyema viungo na walinzi wa Simba. Dr wa Yanga tayari ametoa taarifa ya uwezekano wa 50/50 kuicheza mechi ya kesho baada ya jana kushindwa kufanya mazoezi. Eneo hili Yanga wanaweza kumtumia Juma Saidi ‘ Makapu ‘ akasimama na Thabani Kamusoko. Kamusoko anaweza kushuka na kupanda au kuupoza mpira kati ( holding ) kupunguza pressure ya mpinzani wake ambaye hutegemea zaidi kuichezesha timu tokea kati. Lakini kutokana na Kamusoko kukosa mechi nyingi za ligi hivyo kutokuwa ‘ fit’ sana kwenye game fitness ni lazima viungo wa pembeni na walinzi wa nyuma kwamaana ya full backs wawe na uwezo mkubwa kuuweka mpira mbele ya mstari wa kati pia 7 au 11 mmoja wapo awe na uwezo wa kuingia na kutoka kati kusaidia midfield.

Tambwe anatajwa kupona kuelekea mchezo huu lakini si wa kumtegemea sana , Yusufu Mhilu, Ibrahim Ajibu , Chirwa , Martini na Piusi Buswita wapewe mchezo huu mabegani mwao chini ya nahodha wao Kelvin Yondani. Umakini tu kwa Chirwa kutumia vyema nafasi anazopata maana mwisho wa siku  huwa majuto endapo timu inapoteza au kutoka sare.

Yanga wakitaka kushinda mechi hii ni lazima waingie uwanjani kwa tahadhari kubwa na kuipa Simba heshima yake kama timu ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja kabla ya mechi yao . Hii itawafanya muda wote kuwa makini uwanjani na kufikiria jiinsi gani watavunja au kutibua rekodi hiyo.

Yanga hivi karibuni licha yakuwa na wimbi kubwa la majeruhi na kubadilika mara kwa mara kwa kikosi chao, ushirikiano kitumu uwanjani umekuwa mkubwa pia ni silaha yao kubwa kwa sasa. Wakiweza kusimamia hili watakuwa na nafasi nzuri ya kushinda kesho .

 SAMUEL SAMUEL
28 April 2018

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.