Siri Kubwa Iliyojificha Simba Kuhusiana Na Kasi Ya Upachikaji Mabao



SIMBA wana mzuka kwelikweli kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini kuna siri kubwa imejificha ndani yake kuhusiana na kasi ya upachikaji mabao ya straika wake, John Bocco.


Bocco ameshafunga mabao 12 mpaka sasa huku kasi yake ikizidi kuwa moto na tayari ametoa onyo kwamba, anataka kumalizika msimu akiwa na Kiatu cha Dhahabu.


Lakini, nyuma ya mafanikio ya Simba na Bocco sambamba na kinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara na staa wa Simba, Emmanuel Okwi (16), kuna fundi mmoja anaitwa Shomary Kapombe, ambaye ndiye mpango mzima.


Kuna siri kubwa imejificha kati ya Kapombe, Okwi na Bocco wakilenga kuhakikisha iwe jua au mvua ubingwa msimu huu unatua Msimbazi sambamba na tuzo ya mfugaji bora ili kukata kiu ya mashabiki.


Sasa iko hivi, Kapombe amefichua kuwa wakati akiwa majeruhi kabla ya kurejea uwanjani, waliketi na Bocco na kupanga mikakati ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ili kufikia malengo.


Katika kutekeleza maazimio hayo, Kapombe alirejea kwa mara ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar na akatengeneza nafasi ya bao la pili kwa Bocco.


“Tuna makubaliano na Bocco na Okwi kuhakikisha tunatimiza malengo msimu huu, tunataka ubingwa na tuzo za kutosha ikiwemo Kiatu cha Dhahabu.


“Kuna mechi tisa zimebaki ambazo natakiwa kutengeneza nafasi za mabao za kutosha kwa Bocco ili afikie mabao idadi ya magoli 15 ambayo yanatosha kwa msimu huu wa kwanza na si mbaya akifunga zaidi,” alisema Kapombe.


“Wakati nahangaika na Bocco, pia nina kazi kama hiyo kwa Okwi ambaye anataka kufunga mabao yasiyopungua 20 msimu huu. Kwa kufanya hivyo tutachukua ubingwa na tuzo ya ufungaji na hata mchezaji bora wa kigeni,” alisema.


Simba ambayo inaongoza ligi kwa pointi 49, watacheza na Mtibwa Jumanne pale Jamhuri, Morogoro kisha watarejea Dar es Salaam kwa maandalizi ya Mbeya City na Tanzania Prison.


KUMBE WANAITAKA HESHIMA


Katika hatua nyingine nyota wanne wa Simba Kapombe, Bocco, Erasto Nyoni na Aishi Manula wanaisaka heshima kwa kubeba ubingwa wakiwa na Simba msimu huu, ukiwa ni wa kwanza kwao.


Kapombe alisema walifanya uamuzi mgumu kuondoka Azam, kwa sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wao ikiwemo maslahi madogo.


“Tunaimani itakuwa heshima kwetu kama tukichukua taji na nadhani tutaeleweka kwa nini tuliondoka Azam,” alisema.


Mastaa mzuka kibao


Simba imewazidi mahasimu wao, Yanga kwa pointi tatu na mabao kibao lakini, mastaa Simba wana mzuka kinoma wakiapa kupambana kwa nguvu zote ili kunasa ubingwa.


Manula, ambaye amelifanya lango la Simba kuwa salama msimu huu, amesema pointi tatu ni nyingi sana na, zinawapa mzuka na umakini wa kuongeza bidi zaidi.


“Lengo ni ubingwa na kila mechi iliyopo mbele yetu kwa sasa ni fainali, ndio maana tunaona umuhimu wa kulinda pointi tatu tulizowaacha Yanga,” alisema.


Winga aliye kwenye kiwango bora kwa sasa, Shiza Kichuya amesema wakati huu si wa kulala na kila mchezaji anafikiri kushinda kila mchezo.


“Kama kuna wakati ambapo, akili zinatakiwa kufanya kazi kubwa basi ni sasa.


Mashabiki wetu wamekaa mkao wa kula na tayari wanaiona Simba inakwenda kuwa bingwa.


Unawezaje kuwabadilisha na hii ni changamoto kubwa kwetu ila bidii ni muhimu sana,” alisema
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.