Tambwe Amnyima Usingizi Okwi...


Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi ameanza kuisaka rekodi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara pamoja na ile ya Amiss Tambwe ya mabao 21 msimu wa 2015-16.

Mganda huyo alifunga bao lake la kwanza nje ya Dar es Salaam juzi mjini Shinyanga wakati Simba ilipolazimishwa sare 2-2 na Mwadui na kumfanya kufikisha mabao 14 katika michezo 18 aliyocheza msimu huu.

Okwi ambaye hajawahi kutwaa tuzo ya ufungaji bora nchini tayari ameivunja rekodi yake ya mabao 12 aliyoweka 2011-12, pia ameifikia idadi ya mabao 14 yaliyotoa ufungaji bora msimu uliopita kwa washambuliaji Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting na Simon Msuva wa Yanga msimu wa 2016/17.

Okwi msimu huu amekuwa na wastani wa kufunga bao 1.2 kwa kila mechi aliyocheza na endapo ataendelea kwa kasi hiyo katika michezo 12 iliyobaki basi anaweza kufikia au kuivunja rekodi ya Tambwe.

Tambwe aliweka rekodi ya kufunga mabao 21, katika msimu 2015-16 ikiwa ni mabao mengi zaidi kufungwa kwa msimu mmoja katika kipindi cha miaka 12 iliyopita.

Katika msimu huo, Tambwe aliingoza Yanga kutwaa ubingwa alifuatiwa Mganda Hamis Kiiza wa Simba aliyefunga mabao mabao 19, Mzimbabwe Donald Ngoma wa Yanga (17) na mshambuliaji wa Prisons,Jeremiah Juma (16).
Uwezo mkubwa alionyesha Okwi katika kufunga msimu huu hasa baada ya kuvunja mwiko wa kutofunga nje ya Dar es Salaam unampa nafasi kubwa ya kutwaa kiatu cha dhahabu.

Mganda huyo anatakiwa kufunga mabao sita tu katika michezo 12 iliyobaki ya Simba ili kufikisha magoli 20,sawa na rekodi iliyowekwa na mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma mwaka 2006 alipotwaa tuzo ya ufungaji bora.
Katika michezo 12 iliyobaki ya Simba saba atacheza kwenye Uwanja wa Taifa au Uhuru, Dar es Salaam viwanja ambavyo Okwi amefunga mabao yake 13 msimu huu.

Hivyo rekodi hiyo ya Okwi kwenye viwanja hivyo Dar es Salaam itawalazimu washindani wake wa kubwa katika kuwania tuzo ya ufungaji bora, Obrey Chirwa wa Yanga mwenye mabao 11 na John Bocco wa Simba mabao 10 kufanya kazi ya ziada.

Okwi alisema anachoangalia ni kuipa matokeo timu yake kwanza na ufungaji bora utakuja tu.

“Hakuna ambaye hapendi tuzo lakini muhimu kwanza kwa sasa ni kuisaidida timu yangu kushinda mechi zake zote.
“Ingawa kama itatokea nikamaliza mfungaji bora nitashukuru kwani kila mchezaji anapenda mafanikio lakini itapendeza zaidi kama tutatwaa ubingwa na nikaibuka mfungaji bora,” alisema Okwi.

Kiungo wa zamani wa  Yanga, Sekilojo Chambua alisema Okwi ana nafasi kubwa ya kuibuka mfungaji bora msimu huu kuliko wengine wote labda apate majeraha.

“Okwi ana nafasi ya kuwa mfungaji bora ila anachotakiwa ni kuongeza juhudi ya kufunga hata katika michezo ya mikoani kwani ukiangalia mabao  13 kafunga Dar es Salaam na moja la penalti mkoani.
“Bocco naye anakwenda vizuri ingawa juzi ameumia sasa hapo inategemea kama  atakuwa nje muda mrefu basi moja kwa moja atapoteza nafasi ya kuwania ufungaji bora. Kwa upande wa Chirwa naye  yupo vizuri na anaweza kupata nafasi hiyo ya ufungaji bora ingawa nafasi kubwa zaidi nampa Okwi,” alisema Chambua.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.