Bodi Ya Ligi Yapangua Ratiba Ya Ligi Kuu Tanzania Bara..


Bodi ya ligi kuu Tanzania (TPLB) imepangua tena ratiba ya ligi hiyo kutokana na sababu mbalimbali ambazo zimeshindwa kuzuilika.

Afisa Mtendaji mkuu wa Bodi hiyo, Boniface Wambura amewaambia Waandishi wa habari kuwa moja ya sababu iliyosababisha upanguaji wa ratiba hiyo ni ushiriki wa timu za Simba na Yanga kwenye michuano ya kimataifa.

Mchezo kati ya Simba dhidi ya Stand United ambao ulikuwa ufanyike Machi 4 umerudishwa nyuma siku mbili ili kuwapa nafasi Wekundu hao kujiandaa na mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry.

Mechi kati ya Mtibwa dhidi ya Yanga iliyokuwa ichezwe Machi 3 imeondolewa na itapangiwa tarehe nyingine ili kuwapa nafasi Yanga kujiandaa na mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Township Rolllers ya Botswana Machi 6.

Wambura alisema pia mchezo kati ya Lipuli FC dhidi ya Ndanda imesogezwa mbele kutoka Machi 2 hadi 4 ili kuipa Ndanda muda wa kusafiri kuelekea mkoani Iringa baada ya mechi yao ya kesho dhidi ya Yanga.

Mchezo mwingine uliosogezwa mbele ni kati ya Kagera Sugar dhidi ya Mwadui kutoka Machi 11 hadi 13 ili kuipa Mwadui nafasi kujiandaa na mchezo huo.

"Baada ya mabadiliko hayo ligi itasimama tena Machi 22 kupisha wiki ya FIFA ambapo kutakuwa na mechi za kirafiki za kimataifa.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.