Mo Salah kupelekwa Hispania kwa matibabu
Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah kesho Jumatano atasafirishwa kwenda nchini Hispania kwa ajili ya matibabu ya bega lake, Shirikisho la Soka Misri limesema.
Mfungaji huyo bora wa Liverpool kwa mabao yake 44 alilazimika kutoka uwanjani mapema kwenye mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakifungwa 3-1 na Real Madrid baada ya kuumia bega.
Salah mwenyewe amesema bado anaamini atakuwepo kwenye kikosi cha Misri kwenye Kombe la Dunia nchini Urusi Juni 14, mwaka huu.
Shirikisho la Soka la Misri limesema Salah alianza programu ya matibabu siku ya Jumapili na mambo yalikwenda vizuri kiasi cha kufufua matumaini ya kuwepo kwenye kikosi cha timu yake ya taifa.
Akiwa kwenye matibabu nchini Hispania Salah atakuwa chini ya uangalizi wa Rais wa Shirikisho la Soka la Misri, daktari wa timu ya taifa na mtabibu wa timu ya Liverpool.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.