YANGA YAVAMIA KIGALI KIBABE


YANGA wanatarajia kuondoka kesho jijini Dar es Salaam, kuelekea nchini Rwanda katika Jiji la Kigali kwa ajili ya kucheza mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Rayon Sports huku jina la Straika wao mpya Heritier Makambo likiwa gumzo kubwa nchini humo.
Tofauti na ilivyokuwa ikichukuliwa poa hapo awali, Yanga sasa inatisha kutokana na soka iliyoonyesha, ilipocheza na USM Alger na kuichapa mabao 2-1 huku Makambo akifunga bonge la bao.
Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wanashika mkia katika kundi D lenye timu za Gor Mahia ya Kenya, na USM Alger ya Algeria, zenye pointi nane na Rayon Sport ikiwa na pointi sita, Yanga wakiwa na pointi nne pekee.
Licha ya kwamba hata wakishinda hawatakwenda hatua inayofuata lakini Wanajangwani hao, wamesema iwe jua au mvua lazima waibuke kidedea ili kujenga heshima yao, kwani klabu hiyo ni moja ya timu zenye majina makubwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Taarifa kutoka Rwanda zinasema kuwa, Rayon Sport wamezidi kuingiwa na woga baada ya kufuatilia na kugundua kuwa yupo straika  Makambo ambaye aliwaadabisha USM Alger, Uwanja wa Taifa.
Rayon wanayo nafasi kubwa ya kupenya hatua inayofuata kama watashinda mchezo huo kwani watafikisha pointi tisa huku wakiombea timu moja kati ya Gor Mahia na USM Alger, imfunge mwenzake ili mmoja afikishe hizo pointi tisa na itakayofungwa ibakie na pointi zake nane.
Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, alisema wana Yanga watarajiwe makubwa katika mchezo huo huku akimwagia  sifa Makambo na kubainisha kwamba,   alichokionyesha hadi sasa ni sawa na asilimia 50 na kwamba bado ana ziada nyingine ya kufanya katika mechi zijazo.
“Makambo huyo sio yule ninayemjua, hapa ni kama amecheza asilimia 50 ya uwezo wake, kama atarudi katika ubora wake atakuwa hatari sana na mabeki watamkimbia, ni mchezaji mzuri na anajua nini anafanya akiwa uwanjani,” alisema Zahera.
Akizungumzia mechi hiyo, kocha huyo alisema kikosi chake kipo vizuri na wanakwenda kupambana kuhakikisha wanapata ushindi, pamoja na  kukamilisha ratiba.
“Ni mechi ya kukamilisha ratiba, lakini hatutaki kupoteza, tunahitaji kuendeleza ushindi ili kutuongezea morali ya kufanya vizuri katika michezo yetu ya Ligi Kuu,” alisema.
Yanga wanaondoka wakiwa na ari ya kutosha, baada ya kufanya vizuri katika michezo yao miwili waliocheza hivi karibuni, dhidi ya USM Alger ambao walishinda mabao 2-1 na ule wa Ligi Kuu Tanzania Bara, waliocheza na Mtibwa Sugar na kushinda mabao 2-1, huku Makambo akifunga katika mechi zote.
Mratibu wa timu hiyo Hafidh Saleh, alisema kuwa kikosi chao kikiwa na wachezaji 20 kitaondoka kesho tayari kwa ajili ya mchezo huo wakitumia usafiri wa Ndege.
Alisema huenda wakashindwa kusafiri na wachezaji wawili, Juma Mahadh na Juma Abdul, kutokana na majeraha yanayowasumbua.
Wachezaji hao walipata majeruhi katika mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar uliopigwa Alhamisi

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.